Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema sekta binafsi ina nafasi ya kipekee katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku akiwataka viongozi na watumishi wa umma kubadili mtazamo na kuiona kama mshirika muhimu wa maendeleo badala ya mpinzani.
Akifunga kikao cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za Mkoa wa Dodoma kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Senyamule alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita katika kujenga uchumi unaomilikiwa na Watanzania kupitia uwekezaji wa ndani na ushirikiano imara kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.
"Katika kutekeleza Dira ya Taifa 2050, tutaendelea kupokea wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. Wawekezaji kutoka nje watakuja na mtaji na teknolojia, huku Watanzania wakinufaika kupitia ajira, mapato ya kodi na ukuaji wa uchumi. Hivyo, ni muhimu tubadili mtazamo wetu na kuitambua sekta binafsi kama mshirika wetu wa maendeleo," amesema Senyamule.
Mbali na hilo, Mkuu huyo wa Mkoa amezitaka Halmashauri zote kuhakikisha miradi ya maendeleo ya mwaka wa fedha 2025/2026 ambayo haijakamilika inamalizika kabla ya Oktoba 2026. Pia amesisitiza kukamilishwa kwa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, akieleza kuwa utekelezaji wake umefikia asilimia 98.
Katika eneo la utawala bora, amewataka viongozi kuhakikisha vikao vyote vya kisheria vinafanyika kwa wakati. Amesema Mabaraza ya Madiwani pamoja na Kamati za Maendeleo ya Kata zimefikia utekelezaji wa asilimia 100, huku akibainisha kuwa bado kuna changamoto katika vikao vya maendeleo ya vijiji ambavyo utekelezaji wake umefikia asilimia 70 pekee.
Akizungumzia maandalizi ya Samia Day 2026, Senyamule amesema maadhimisho ya mwaka huu yanatarajiwa kuwa makubwa zaidi kutokana na mafanikio yaliyopatikana mwaka 2025, ambapo zaidi ya wananchi milioni 1.7 walipata fursa ya kufahamu utekelezaji wa miradi na mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika ngazi ya kata.
Aidha, amesema maadhimisho hayo yataambatana na kampeni ya uhamasishaji kuhusu Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), yatakayofanyika kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda, ikiwa ni sehemu ya kuwajengea wananchi uelewa na hamasa ya kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya mashindano hayo.








Comments
Post a Comment