Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF), Jenerali Jacob John Mkunda amelitaka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kulinda amani na mipaka ya Taifa, ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama na yenye utulivu.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa kilele cha Mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF CUP 2026), Jenerali Mkunda alisema michezo ni sehemu muhimu ya kujenga afya, mshikamano na utayari wa wanajeshi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Mashindano hayo yalihitimishwa kwa mchezo wa fainali uliowakutanisha DFHQ na JKT, ambapo timu ya JKT iliibuka bingwa baada ya kuifunga DFHQ kwa mabao 3-1 katika mchezo ulioshuhudiwa na viongozi mbalimbali wa jeshi pamoja na wadau wa michezo.
Aidha, Jenerali Mkunda amewaasa wanamichezo hao kuendelea kujitunza, kujiweka katika kiwango bora cha utimamu wa mwili na kuzingatia nidhamu pamoja na sheria za michezo wanaposhiriki mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Majeshi amezitaka timu zote za kijeshi nchini kuweka mikakati endelevu ya kutambua na kuendeleza vipaji vya vijana wenye uwezo wa michezo ili kujiunga na JWTZ na kuhakikisha kunakuwa na mwendelezo wa wanamichezo wenye uwezo mkubwa pindi wengine wanapostaafu au kumaliza muda wao wa kushiriki mashindano.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano hayo, Brigedia Jenerali Saidi Hamis Saidi, amesema malengo ya CDF CUP 2026 yamefikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana na ushiriki mzuri wa wanamichezo wa vikosi mbalimbali na kufanikiwa kuibua vipaji vipya vinavyoweza kuendelezwa.
Amesema mashindano hayo yameendelea kuwa chachu ya kuimarisha mshikamano, ushirikiano na kubadilishana uzoefu miongoni mwa wanajeshi, huku yakitoa nafasi ya kuibua vipaji vitakavyowezesha JWTZ kupata wanamichezo bora wa kuiwakilisha taasisi hiyo katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Mashindano ya CDF CUP 2026 yamefungwa kwa mafanikio makubwa, huku uongozi wa JWTZ ukisisitiza kuwa utaendelea kuyaimarisha ili yawe jukwaa la kuibua vipaji, kukuza michezo na kuendelea kujenga jeshi lenye afya bora, nidhamu na utayari wa kutekeleza wajibu wake wa kulinda Taifa.














Comments
Post a Comment