Watumiaji wa mafuta nchini wameanza mwezi Julai kwa nafuu baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kutangaza kupungua kwa bei kikomo za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kufuatia kushuka kwa bei katika soko la dunia.
Akitoa taarifa kwa umma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Gerald Maganga, amesema kuanzia Julai 1, 2026, bei za petroli zitashuka kwa Shilingi 96 kwa lita, dizeli kwa Shilingi 151 kwa lita, huku mafuta ya taa yakishuka kwa Shilingi 242 kwa lita.
Amesema mabadiliko hayo yamechochewa na kuanza kutulia kwa mwenendo wa soko la mafuta duniani baada ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Iran kuhusu mvutano wa Mashariki ya Kati ambapo Makubaliano hayo yameruhusu meli za mafuta kuendelea kupita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, hatua iliyosaidia kupunguza changamoto za usafirishaji wa mafuta duniani.
Aidha, kampuni za kusafisha mafuta ghafi zimeendelea kununua mafuta kutoka maeneo mengine yasiyoathiriwa na vita ili kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea bila usumbufu.
Pamoja na hali hiyo kuleta nafuu, EWURA imeeleza kuwa bei za mafuta katika soko la dunia bado hazijarudi kwenye kiwango kilichokuwepo kabla ya kuanza kwa vita mwishoni mwa Februari 2026.
Bei hizo mpya zimeanza kutumika rasmi kuanzia saa 6:01 usiku wa Julai 1, 2026, kwa mujibu wa bei kikomo zilizotangazwa na EWURA kwa mikoa yote nchini. .
Mamlaka hiyo imewataka wafanyabiashara wa mafuta kuuza bidhaa zao kwa kuzingatia bei hizo, ikisisitiza kuwa ukiukwaji wa maelekezo hayo utachukuliwa hatua kali za kisheria.
EWURA imewahimiza wananchi kufuatilia bei kikomo katika maeneo yao kwa kupiga 15200# kupitia simu za mkononi bila malipo. Pia imevitaka vituo vyote vya mafuta kuweka wazi mabango ya bei, kutoa stakabadhi za kielektroniki (EFPP) kwa kila mnunuzi na kuendesha biashara kwa kuzingatia sheria ili kulinda haki za watumiaji na kuimarisha ushindani wa soko.
Hatua hiyo inatarajiwa kuwapunguzia wananchi na sekta mbalimbali za uzalishaji gharama za matumizi ya mafuta, huku ikitoa matumaini ya kuendelea kwa utulivu wa bei endapo mwenendo wa soko la dunia utaendelea kuimarika.

Comments
Post a Comment