RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Kesho Julai mosi, 2026, anatarajiwa kutoa rasmi Tuzo za Rais kwa Walipakodi Bora kwa walipakodi waliokidhi vigezo vilivyowekwa, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mlipakodi yanayolenga kuhamasisha utamaduni wa kulipa kodi nchini na kutambua mchango wao mkubwa katika maendeleo ya taifa.
Maadhimisho hayo yanaenda sambamba na kumbukumbu ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Julai 1, 1996, yakidhihirisha mafanikio ya ushirikiano uliojengwa kati ya TRA na walipakodi kwa kipindi cha miongo mitatu katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuchangia maendeleo ya sekta mbalimbali nchini.
Katika kipindi hicho chote cha miaka 30, TRA imeendelea kushirikiana kwa karibu na walipakodi, huku ikiwashukuru kwa kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati, jambo lililowezesha Serikali kupata rasilimali za kugharamia maendeleo ya nchi.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya miaka 30 ya TRA ni, "Kulipa Kodi ni Uzalendo na Ushujaa kwa Maendeleo na Kujitegemea kwa Taifa Letu," ikiwa ni wito kwa Watanzania kuendelea kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari ili kuendeleza maendeleo ya taifa.

Comments
Post a Comment