MBUNGE wa Jimbo la Serengeti, Mheshimiwa Mary Daniel Surati, amehitimisha kwa mafanikio awamu ya kwanza ya programu ya Samia Uthubutu Awards na kuzindua rasmi awamu ya pili ya mpango huo unaolenga kuibua vipaji, kukuza ubunifu na kuwajengea wanafunzi uwezo wa kufikiri kwa ubunifu ili kuwa sehemu ya maendeleo ya Taifa.
Programu hiyo ilitekelezwa katika shule 30 za sekondari, zikiwemo shule 25 za Wilaya ya Serengeti na 5 za Wilaya ya Tarime, ambapo wanafunzi walishindana kupitia mawazo na bunifu mbalimbali zilizoonesha uwezo wao wa kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.
Katika mashindano hayo, Makundusi Sekondari iliibuka mshindi wa kwanza na kujinyakulia Shilingi 1,000,000, kombe, vyeti vya ushindi pamoja na fursa ya kipekee ya kutembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mary Surati amesema yeye mwenyewe atawaongoza washindi hao katika ziara hiyo ya kielimu ili kuwapa nafasi ya kujifunza shughuli za Bunge na uongozi wa nchi.
Nafasi ya pili ilikwenda kwa SEDECO Sekondari, iliyopata Shilingi 800,000, kombe na vyeti, huku Matongo Sekondari ya Wilaya ya Tarime ikishika nafasi ya tatu na kujishindia Shilingi 500,000, kombe na vyeti vya kutambua ubunifu wao.
Mbali na washindi wakuu, shule zote zilizoshiriki zilitunukiwa vyeti vya ushiriki ikiwa ni ishara ya kuthamini juhudi zao.
Aidha, wanafunzi wote walioshiriki wameahidiwa fursa ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ziara inayolenga kuwapa elimu kuhusu uhifadhi wa maliasili na nafasi ya utalii katika kukuza uchumi wa Tanzania.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mheshimiwa Mary Surati alisema programu ya Samia Uthubutu Awards inalenga kuwajengea vijana ujasiri, ubunifu na uwezo wa kutumia vipaji vyao kutengeneza fursa za maendeleo, sambamba na kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwekeza katika elimu na maendeleo ya vijana.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Alex Choya Choya, Mkuu wa Idara ya Utalii wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambaye aliwataka wanafunzi kuendelea kutumia ubunifu wao kama chachu ya maendeleo ya taifa na kutunza rasilimali za nchi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Programu hiyo ilifanyika chini ya kaulimbiu isemayo: "Ubunifu wa Vijana, Nguvu Kazi ya Taifa," ikiwa ni wito wa kuhamasisha vijana kutumia maarifa na vipaji vyao katika kujenga Tanzania yenye maendeleo na ushindani.


Comments
Post a Comment