*Na: Dawati la Habari Polisi Mwanza*
-Wananchi Misungwi wadai mitandao ya kijamii inadhoofisha maadili ya vijana, Polisi waahidi kuwachukulia hatua wahalifu wa mtandaoni
Baadhi ya wananchi mkoani Mwanza wameiomba Serikali kuimarisha udhibiti wa matumizi ya mitandao ya kijamii kwa kuweka mikakati madhubuti ya kisheria, wakieleza kuwa baadhi ya matumizi yake yameanza kuhatarisha maadili ya vijana na kuchochea taharuki katika jamii.
Ombi hilo limetolewa na Katibu wa Maafisa Usafirishaji wa Kata ya Usagara, Wilaya ya Misungwi, Thomas Michael, wakati wa mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto za kiusalama katika eneo hilo.
Katika mkutano huo uliowahusisha wananchi pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa, Michael alisema licha ya manufaa ya mitandao ya kijamii, baadhi ya watumiaji wamekuwa wakiitumia vibaya kwa kusambaza taarifa zisizo sahihi na maudhui yanayodhoofisha maadili ya vijana.
"Tunaomba kama kuna uwezekano wa kuidhibiti hii mitandao ya kijamii muweze kuidhibiti kwani imekuwa ikileta taharuki katika jamii. Pia imekuwa chanzo cha vijana wengi kuharibika kiakili, hivyo Serikali iweze kuchukua hatua," alisema Michael.
Akijibu hoja hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, alisema Jeshi la Polisi linaendelea kufuatilia kwa karibu matumizi ya mitandao ya kijamii kupitia wataalamu wa makosa ya mtandao na kuwachukulia hatua wale wanaokiuka sheria.
Alisema baadhi ya watu tayari wamekamatwa kwa makosa mbalimbali yanayohusiana na matumizi mabaya ya mitandao, ikiwemo wizi na makosa mengine ya jinai, huku wengine wakifikishwa mahakamani.
"Wapo ambao tumekuwa tukiwakamata kwa makosa mbalimbali ikiwemo makosa ya wizi. Wapo ambao wameshikwa na wengine wamefikishwa mahakamani," alisema DCP Mutafungwa.
Aliongeza kuwa hakuna mtu anayefanya uhalifu mtandaoni ambaye yuko salama, kwani sheria zimeweka utaratibu wa kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
"Sheria ipo wazi na inaeleza utaratibu wa kuwashughulikia wale wanaofanya makosa hayo. Wananchi waache vitendo hivyo kwa sababu Jeshi la Polisi linaendelea kufanya ufuatiliaji kwa weledi mkubwa," alisema.
Polisi yaendelea na doria
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Misungwi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Gasper Silayo, aliwataka wananchi kuendelea kudumisha amani na kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kila mmoja aweze kufanya shughuli zake kwa utulivu.
Aliwataka wananchi kuwa wazalendo, kulinda miundombinu ya umma na kuzingatia sheria, huku akisisitiza umuhimu wa madereva kufuata sheria za usalama barabarani.
"Wajibu wetu Jeshi la Polisi ni kusimamia sheria. Kwa mujibu wa sheria, hairuhusiwi mtu kuendesha chombo cha moto na kuingia barabarani bila kuwa na leseni," alisema SSP Silayo.
Wananchi waomba kituo cha polisi
Katika mkutano huo, Diwani wa Kata ya Usagara, Erasto Kashinje, aliomba radhi kwa niaba ya wananchi kuhusu tukio la kuchomwa moto kwa kituo cha Polisi Nyashishi wakati wa vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025.
Alisema wananchi wako katika hatua za mwisho za kukamilisha ujenzi wa kituo kipya cha Polisi Usagara chenye hadhi ya Daraja "C", hatua ambayo itasaidia kusogeza huduma za usalama karibu na wananchi.
Mkazi wa Nyashishi, Janeth Evalista, alisema uwepo wa kituo cha polisi katika eneo hilo ni muhimu kutokana na changamoto zinazowakabili vijana, ikiwemo kuongezeka kwa matumizi ya pombe na michezo ya kamari.
"Ninaomba uwepo wa kituo cha Polisi cha dharura hapa kwetu. Ukiangalia vijana wengi sasa wamejiingiza kwenye ulevi na michezo ya kamari; swali la kujiuliza ni je, hizi pesa wanazipata wapi?" alihoji.








Comments
Post a Comment