ENG. MWANAISHA ULENGE AFUNIKA JIJI LA TANGA, ATUMIA MILIONI 170 KUGAWA MIGUU BANDIA, VIGOGO WAMWAGIA SIFA
📍 Waziri wa Fedha aonya watu wanaochezea Amani ya nchi
Na Mashaka Mhando, Tanga
JIJI la Tanga limetikisika kufuatia tukio la kihistoria la matendo ya huruma lililofanywa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tanga, Mhandisi Mwanaisha Ulenge, baada ya kumwaga kiasi cha Shilingi Milioni 170 kutoa vifaa saidizi, ikiwemo miguu bandia, na kurejesha tabasamu kwa mamia ya watu wenye ulemavu.
Tukio hilo kubwa ambalo limeacha gumzo jijini Tanga, limefanyika Julai 14 mwaka huu, ambapo Mhandisi Ulenge, kupitia taasisi yake ya Ng'arisha Maisha Foundation akishirikiana na Kamal Foundation, aligawa viti mwendo (Wheelchairs) 31, miguu bandia 100, na fimbo 25 kwa walemavu. Mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar.
Kitendo hicho cha kiutu kimeonekana kuwagusa viongozi mbalimbali waandamizi wa kisiasa. Mwanasiasa mkongwe nchini, Mama Mwantumu Mahiza, sambamba na Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Tanga, Moza Shilingi, walisimama na kuahidi kumuunga mkono kwa dhati Mhandisi Ulenge katika harakati zake.
Akipongeza hatua hiyo, Mama Mwantumu alisema: "Unapokuwa Mbunge na kuigusa jamii katika mazingira ya namna hii ya uhitaji mkubwa, ni kuendelea kubarikiwa. Huu ndio uongozi wenye kuacha alama."
Falsafa ya Kuacha Alama na Dira 2050
Katika risala yake iliyogusa hisia za wengi, Mhandisi Ulenge aliweka wazi dhamira yake ya dhati akibainisha kuwa kiongozi bora ni yule anayetengeneza njia na kuwasaidia wanyonge.
"Ng'arisha Maisha ni taasisi ya kitaifa isiyo ya kiserikali niliyoianzisha mwaka 2021... Kiongozi mzuri ni yule anayeacha alama. Nataka kuacha alama kwenye ardhi hii nitakayozikwa,"* alisema Mhandisi Ulenge huku akishangiliwa.
Aliongeza kuwa taasisi yake inamuunga mkono kwa vitendo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza Malengo Endelevu na Dira ya 2050, inayosukumwa na kaulimbiu ya “Yeyote asiachwe nyuma (No one left behind).”
Ili kuwafanya walemavu hao waweze kujitegemea kiuchumi, kabla ya kukabidhiwa vifaa hivyo, walipatiwa mafunzo maalum na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ili waweze kuchangamkia fursa za tenda za Serikali zinazotengwa maalum kwa ajili ya makundi maalum.
Ulenge Ambana Waziri wa Fedha Kuhusu Barabara
Akitumia vyema uwepo wa Waziri wa Fedha kwenye hafla hiyo, Mhandisi Ulenge alimkabidhi faili la miradi ya kimkakati ya Mkoa wa Tanga inayohitaji fedha za haraka.
Aliiomba Serikali kutoa fedha kwa ajili ya barabara ya Tanga - Pangani na kutatua changamoto za fidia, ujenzi wa barabara ya Handeni - Kibirashi - Chemba - Kwamtoro hadi Singida, pamoja na barabara ya mchepuko (Bypass) ya Kiomoni - Mlingano, akisisitiza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutatimiza ndoto za Rais Samia za kuifungua Tanga.
Waziri Omar Aonya Kuhusu Amani
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha Balozi Khamis Omar alimwagia sifa Mhandisi Ulenge kwa kurudisha utu wa watu hao na kuwaondolea hofu ya maisha. Waziri huyo alitumia jukwaa hilo kutoa angalizo zito kuhusu umuhimu wa kulinda amani.
"Niwaombe tuendelee kudumisha amani yetu. Inapovunjika amani wanaweza kupatikana walemavu wengi sana. Tunaweza kutofautiana kwa mawazo, lakini isiwe sababu ya kuhitilafiana na kuvunja amani yetu ambayo ndio msingi wa maendeleo," alionya Waziri Omar.
Vigogo Wengine Wanena
Hafla hiyo ilihudhuriwa na vigogo mbalimbali waliopongeza hatua hiyo:
* Meja (Mst) Hamisi Mkoba (Mwenyekiti CCM Wilaya Tanga): Alielezea msaada huo kama sadaka yenye thamani kubwa kwa jamii na mbele za Mwenyezi Mungu.
* Hajat Sheymar Kweigir (Mwenyekiti UWT Mkoa wa Tanga): Alikiri kuguswa sana na tukio hilo, akikumbushia namna matendo hayo yalivyo na thamani akiwa kama Mbunge mstaafu.
* Mhe. Dadi Kolimba (DC Tanga): Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, aliwataka wadau na wanasiasa wengine kuiga mfano huo wa vitendo ulioonyeshwa na Mhandisi Ulenge.
Kwa upande wa wafadhili waliowezesha mradi huo kwa kushirikiana na Ng'arisha Maisha, Mkurugenzi wa Kamal Foundation, Sameer Santosh Gupta, aliahidi kuendelea kushirikiana na Serikali inayoongozwa na Rais Samia kutokana na mazingira rafiki yaliyowekwa kwa sekta binafsi, akilenga kujenga jamii yenye usawa.







Comments
Post a Comment