Akifungua mafunzo ya wabunge hao yaliyoandaliwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) leo Jun 16,2026 jijini Dodoma, Spika Zungu amesema bado kuna dhana potofu zinazowazuia wananchi wengi kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi, hivyo akawataka wabunge kuwa mabalozi wa mabadiliko hayo katika maeneo yao.
Amesema baadhi ya wananchi wanaamini kimakosa kuwa nishati safi ni ghali, ngumu kutumia na huathiri ladha ya chakula, jambo ambalo si la kweli.
Sambamba na hayo amewataka wabunge hao kwenda kwa wananchi na kutoa elimu sahihi ili kuondoa mitazamo hiyo na kusaidia kufikia lengo la Serikali la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Steven Kiruswa, amesema STAMICO imeendelea kuwa sehemu muhimu ya suluhisho la changamoto za nishati kupitia uzalishaji wa mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes, ambao ni rafiki kwa mazingira na wenye gharama nafuu kwa watumiaji.
Dkt. Kiruswa ameleza kuwa matumizi ya mkaa huo wa kisasa yanasaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa wa miti, huku yakichangia kupunguza magonjwa ya macho na mfumo wa upumuaji yanayotokana na moshi wa nishati za jadi.
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa STAMICO, Baraka Manyama amesema shirika hilo linaendelea na mkakati wa kupanua uzalishaji wa Rafiki Briquettes kwa kuongeza viwanda zaidi nchini.
Amebainisha kuwa hatua hiyo inalenga kukidhi mahitaji ya soko la ndani na kufungua fursa za kuuza bidhaa hiyo katika masoko ya kimataifa.
STAMICO imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha matumizi ya nishati safi yanaenea kwa kasi nchini, hatua inayotarajiwa kuleta manufaa makubwa katika afya, mazingira na maendeleo ya uchumi wa wananchi.




Comments
Post a Comment