📍Aishauri Serikali kutouogopa mfumo wa Idras ili nchi ijitegemee kwa bajeti kwa asilimia 100 bila mikopo
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MBUNGE wa Mkinga, Mheshimiwa Twaha Said Mwakioja, ameitaka Serikali kubadilisha mifumo ya kodi na kupeleka mabilioni ya kilimo moja kwa moja kwa wananchi vijijini.
Ametoa mchango huo mzito wa kiuchumi leo bungeni jijini Dodoma wakati akichangia hotuba ya Serikali, huku akijikita katika maeneo makuu mawili ya dharura: Dira ya Taifa ya Maendeleo na Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani.
Dira ya 2050 na Mageuzi ya Kilimo
Mheshimiwa Mwakioja alibainisha kitalamu kuwa Dira ya 2025 inayoelekea ukingoni ilikuwa nzuri kiuandishi, lakini imeshindwa kufikia lengo la kuondoa umasikini wa chakula kwa asilimia 0, kwani takwimu za sasa zinaonyesha umasikini huo bado umeganda asilimia 8.
Ameishauri Serikali kuelekea Dira mpya ya 2050, nchi inahitaji uchumi jumuishi na shirikishi utakaofuta umasikini vijijini kwa asilimia 100, huku nguzo kuu ikiwa ni Kilimo, Ufugaji, na Uvuvi. Alimpongeza kwa dhati Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mbadilishaji wa sekta hizi kwa kuongeza bajeti kutoka Shilingi bilioni 200 hadi wastani wa Trilioni 1.
Hata hivyo, Mhe. Mwakioja alihoji ni kwanini kasi ya kupunguza umasikini mtaani ni ndogo sana (mabadiliko ya 1.3% pekee) wakati uchumi wa taifa unakua kwa kasi.
"Fedha hizi nyingi za Rais zisiishie kwenye maandiko huko maofisini; ziende moja kwa moja kwa mkulima, mfugaji, na baharini ili kuleta matokeo ya haraka," alisisitiza Mhe. Mwakioja.
Mapinduzi ya Mapato: Idras na ETS
Katika eneo la mapato, Mbunge huyo ametoa mapendekezo mazito yanayogusa mifumo miwili ya dharura ili kukuza uchumi wa nchi, Moja alipendekeza mfumo wa Idras kusoma uchumi wote, kurudisha e-invoice, kuruhusu risk profiling na kupanua kodi katika sekta isiyo rasmi. Kupandisha mapato ya nchi kutoka Trilioni 3 hadi Trilioni 5 au 6 kwa mwezi (Ndani ya miaka 3-5).
Pili alisema mfumo wa ETS Mzabuni apewe mkataba mrefu (miaka 5-10) na asukumwe kujenga kiwanda ndani ya nchi. Kushusha gharama za teknolojia, kuzalisha ajira kwa vijana, na kudhibiti bidhaa bandia.
Mhe. Mwakioja alifafanua zaidi kuwa ili wigo wa kodi upanuke mtaani, mfumo wa stempu za kielektroniki (ETS) unapaswa kuongezwa nguvu na kuanza kutumika kwenye bidhaa zingine za kimkakati kama Saruji (Cement), Mafuta ya kula, Sukari, na Ngano.
Alihitimisha kwa kutoa wito mzito kwa Serikali na wanasiasa wenzake kutouogopa mfumo wa Idras, na badala yake waufumbatie na kuusimamia kidhati ili nchi iweze kugharamia bajeti yake kwa asilimia 100 bila kutegemea mikopo au misaada inayoendelea kupungua nyanjani.



Comments
Post a Comment