Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetoa fursa ya mwisho kwa vijana waliohitimu Kidato cha Sita mwaka 2026 na kuchaguliwa kujiunga na Mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria, lakini wakashindwa kuripoti katika makambi waliopangiwa awali, kuripoti katika makambi yaliyo karibu na maeneo wanayoishi kuanzia Juni 12 hadi Juni 15, 2026.
Akitoa taarifa hiyo leo Juni 12, 2026 katika Makao Makuu ya JKT Chamwino jijini Dodoma, Mkuu wa Tawi la Operesheni na Mafunzo JKT, Brigedia Jenerali Peter Mnyani, amesema hatua hiyo inatekeleza maelekezo ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Nduku Mabele, ya kuhakikisha vijana wote waliochaguliwa wanapata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo muhimu ya uzalendo, uzingatiaji wa sheria na ujenzi wa taifa.
Amesema awali JKT liliwataka vijana hao kuripoti katika makambi waliopangiwa kuanzia Juni 1 hadi Juni 7, 2026, lakini baadhi yao walishindwa kufanya hivyo kutokana na sababu mbalimbali.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa JKT ameelekeza vijana wote ambao bado hawajaripoti kwenda katika makambi ya JKT yaliyo karibu na maeneo yao ya makazi ili kuendelea na utaratibu wa kujiunga na mafunzo.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa utaratibu huo hauhusishi Kambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandizi mkoani Pwani, Kambi ya Makutupora JKT mkoani Dodoma pamoja na Chuo cha Uongozi cha JKT (CUJKT) kilichopo Kimbiji jijini Dar es Salaam.
Vijana hao wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia leo tarehe 12 Juni 2026 hadi tarehe 15 Juni 2026 bila kukosa.





Comments
Post a Comment