Na Mwandishi wetu Jovina Massano
Waganga wa tiba asili na mbadala hapa nchini washauriwa kusalimisha na kusajili nyara wanazotumia katika shughuli zao ili kuepuka adhabu na kukamatwa.
Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Umoja wa Machifu Tanzania Mtemi Nyamilonda wa tatu Harun Mkomangwa jijini Mwanza mbele ya Mhifadhi mkuu Kituo Cha TAWA Mwanza kamanda Venance Mkamwa wakati wa zoezi la utoaji elimu ya uhifadhi iliyotolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori Tanzania (TAWA).
Mtemi Nyamilonda wa tatu amesema kumiliki nyara kihalali kutasaidia kuepuka adhabu za kukamatwa na faini kwa watumiaji zitakazopelekea kuwaondolea hofu katika uteketezaji wa majukumu yao.
Aidha amewasisitiza viongozi walioshiriki katika zoezi hilo la elimu kuhakikisha wanawaelimisha waganga wa tiba asili na mbadala ambao hawakuweza kufika ili nao waweze kunufaika na umiliki nyara kihalali na kufuata miongozo taratibu na sheria zilizowekwa.
"Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuweza kutusikiliza na kuhakikisha imeweka utaratibu maalum wa kuwezesha upatikanaji wa nyara na vibali vya umiliki kwa wakati hii inaonyesha dhahiri ushirikiano na viongozi wa mila na desturi zilizo njema hapa nchini", amesema Mtemi Nyamilonda.
Jitihada hizi ni mojawapo ya hatua inayowarahisishia waliomiliki nyara kwa kirithi kupata uhalali wa umiliki.
Umiliki wa halali kutawawezesha waganga wa tiba asili na mbadala wataondokana na kadhia ya kukamatwa na kufanya kazi zao kwa amani.
Sanjari na hayo Mtemi Nyamilonda ameiomba Serikali upatikanaji wa nyara uendelee kuwa wazi na utangazwe zaidi kupitia vyombo vya habari ili wanaohitaji wapate kwa wingi lakini pia ameomba wigo uongezwe katika mikoa yote na uwekwe utaratibu maalum wa umiliki ili walio na nia ovu wasizitumie vibaya.
Nao waganga wa tiba asili na mbadala wamekiri kuwepo kwa changamoto ya kukamatwa lakini wameishukuru TAWA kwa kuwaelimisha na kuwafafanulia namna ya kumiliki nyara kihalali wameahidi kuwa mabalozi kwa wengine.
Hata hivyo Mtemi Nyamilonda wa tatu amependekeza kuwa waganga wa tiba asili na mbadala wanaohitaji wapate nyara wafike na barua ya utambulisho kutoka kwa wazee wa mila na machifu waliopo katika maeneo yao ili matumizi ya nyara yatumike kwa waganga halisi.
Hii inatokana na uwepo wa waganga wa tiba asili na mbadala wasio halali wanaojihusisha na uganga ilihali hawana kalama hiyo na wamepewa leseni za tiba asili na ndio wanaojihusisha na ramli chonganishi amemalizia Mtemi Nyamilonda wa tatu.



Comments
Post a Comment