Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, biashara na uwekezaji ili kuongeza manufaa kwa wananchi wa mataifa hayo mawili kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kupitia makubaliano hayo, yalitofanyika mapema hii leo June 9, Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais samia ameeleza kuwa licha ya ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na Singapore, kiwango cha sasa cha dola milioni 299 za Marekani bado hakijafikia matarajio ya pande zote.
Kwa sasa Singapore imewekeza katika miradi 36 nchini Tanzania, huku makubaliano yaliyofikiwa yakilenga kuongeza uwekezaji, biashara na fursa mpya za ushirikiano katika sekta mbalimbali za uchumi.
Tanzania pia imeiomba Singapore kufungua ubalozi wake nchini ili kuimarisha zaidi mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi, pamoja na kuanzisha mfumo wa mashauriano ya mara kwa mara kwa ajili ya kuratibu maeneo ya ushirikiano.
Katika sekta ya kilimo, nchi hizo zimeonyesha nia ya kushirikiana kuimarisha usalama wa chakula, hatua itakayoongeza fursa za biashara ya mazao na kuhakikisha upatikanaji wa chakula kwa uhakika.
Kwa upande wake, Rais wa Singapore Tharman Shanmugaratnam amesema kuwa Biashara na minyororo ya ugavi duniani unaendelea kupitia mabadiliko makubwa yanayosababishwa na mvutano wa kisiasa, migogoro ya kimataifa na changamoto nyingine za kiuchumi. Wakati huohuo, athari za mabadiliko ya tabianchi zinazidi kuongezeka, huku nchi zinazoendelea zikikabiliwa na hatari ya kubeba mzigo mkubwa wa mabadiliko hayo kwa masharti yanayowekwa na mataifa yenye nguvu zaidi kiuchumi.
Hali hiyo imeendelea kuibua umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa unaojengwa katika misingi ya uwazi, usawa na manufaa ya pamoja. Mahusiano kati ya Afrika na Asia yameelezwa kuwa na nafasi muhimu katika kufungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi kwa mataifa ya pande zote mbili, hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya haraka ya mfumo wa biashara duniani.
Katika kuendeleza azma hiyo, Tanzania na Singapore zimechukua hatua za vitendo za kuimarisha ushirikiano wao wa kiuchumi kwa lengo la kuchochea ukuaji wa biashara na uwekezaji kati ya kanda za Afrika Mashariki na Asia ya Kusini-Mashariki. Hatua hizo zinatarajiwa kuongeza mtiririko wa mitaji, teknolojia na fursa za kibiashara, huku nchi hizo zikijijengea nafasi muhimu kama lango la biashara katika maeneo yao husika.











Comments
Post a Comment