Serikali imeeleza mpango wake wa kuendelea kuisaidia Halmashauri ya Wilaya ya Butiama katika jitihada za kuboresha miundombinu ya biashara, hususan ujenzi wa soko katika eneo la Kiabakari, linalokua kwa kasi kiuchumi.
Akijibu swali la Mbunge wa Butiama, Mheshimiwa Charles Mahera leo Jun 9,2026 Bungeni Jijini Dodoma,Naibu Waziri wa TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema kuwa Butiama ni miongoni mwa halmashauri zenye mapato ya ndani ya chini, hivyo Serikali inaendelea na mkakati wa kuziwezesha halmashauri hizo kuongeza vyanzo vya mapato.
Dkt. Dugange amebainisha kuwa eneo la Kiabakari tayari limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa soko, ambalo litakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi, hususan wanawake wanaojishughulisha na biashara katika eneo hilo, pamoja na kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri.
Aidha, Serikali imeitaka Halmashauri ya Butiama kuanza kutenga fedha ndani ya bajeti yake kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa soko hilo, huku ikiahidi kuendelea kusaidia mradi huo kadri ya upatikanaji wa bajeti za maendeleo.
“Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za halmashauri, ili kuhakikisha soko hilo linakamilika na kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema Naibu Waziri.
Mradi huo unatarajiwa kuwa chachu ya kukuza shughuli za kiuchumi katika eneo la Kiabakari na kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri ya Butiama.



Comments
Post a Comment