SERIKALI imeweka mkazo katika kuongeza mapato ya ndani na kuimarisha uchumi wa kujitegemea kupitia utekelezaji wa mikakati mipya ya ukusanyaji kodi, huku ikitangaza kuanzishwa kwa Programu ya Tuzo ya Uzalendo itakayowazawadia wananchi na wafanyabiashara wanaoshiriki kikamilifu katika matumizi ya risiti za kielektroniki.
Akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Dkt. Khamis Mussa Omar, amesema Serikali itaendelea kupunguza utegemezi wa misaada na mikopo ya nje kutokana na changamoto zinazoendelea kujitokeza ikiwemo kupungua kwa misaada ya maendeleo na kuongezeka kwa gharama za mikopo.
Amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali itatekeleza hatua mbalimbali za kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani, zikiwemo kuvutia uwekezaji wa ndani na nje, kupanua wigo wa kodi, kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na walipakodi, pamoja na kusimamia matumizi sahihi ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD).
Aidha, Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA kwa kutumia teknolojia za kisasa za Akili Unde (AI) na uchambuzi wa taarifa kubwa (Big Data), hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi katika usimamizi na ukusanyaji wa mapato pamoja na kuziba mianya ya upotevu wa fedha za umma.
Waziri Omar amebainisha kuwa Serikali pia itaimarisha usimamizi wa taasisi za umma ili kuongeza tija katika ukusanyaji wa maduhuli, kuhakikisha gawio na michango ya Serikali inawasilishwa kwa wakati, pamoja na kuhimiza matumizi ya msimbopau (barcode) kwa bidhaa zote zinazozalishwa, kuagizwa na kuuzwa ndani na nje ya nchi.
Vilevile, Serikali imepanga kuanza kutekeleza baadhi ya mapendekezo 284 yaliyotolewa na Tume ya Rais ya Maboresho ya Mfumo wa Kodi kwa lengo la kujenga mfumo wa kodi wenye ufanisi zaidi na unaochochea ukuaji wa uchumi.
Katika hatua nyingine, Serikali itazindua Julai 2026 Programu ya Tuzo ya Uzalendo kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Risiti za Kielektroniki, ambapo washiriki watakaodai au kutoa risiti halali watapata fursa ya kushinda zawadi mbalimbali kupitia droo za bahati nasibu.
Hatua hiyo inalenga kujenga utamaduni wa kudai na kutoa risiti stahiki, kuongeza uwajibikaji katika biashara na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.

Comments
Post a Comment