SERIKALI imesema deni la Taifa linaendelea kuwa himilivu na salama licha ya kufikia shilingi trilioni 114.34 hadi Machi 2026, kutokana na usimamizi madhubuti wa deni na matumizi ya mikopo katika miradi ya maendeleo yenye tija kwa uchumi wa nchi.
Akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema kati ya deni hilo, shilingi trilioni 38.45 ni deni la ndani sawa na asilimia 33.6, huku shilingi trilioni 75.89 zikiwa ni deni la nje sawa na asilimia 66.4.
Amesema mikopo hiyo imeelekezwa katika sekta za kimkakati zinazochochea ukuaji wa uchumi, ikiwemo miundombinu ya usafirishaji, nishati na mawasiliano.
Kwa mujibu wa tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Novemba 2025, viashiria vyote vya deni vinaendelea kubaki ndani ya viwango vya kimataifa vinavyokubalika, jambo linaloonesha uwezo wa Tanzania kuhimili deni lake bila kuhatarisha uthabiti wa uchumi.
Waziri Omar amesema tathmini za mwaka 2026 zilizofanywa na kampuni za kimataifa za Moody's na Fitch Ratings zimeonesha Tanzania ina uwezo mzuri wa kukopa na kulipa madeni yake, kutokana na ukuaji wa uchumi, maboresho ya mazingira ya biashara na uwekezaji, pamoja na nidhamu katika matumizi ya fedha za umma.
Aidha, Tanzania imeibuka mshindi wa jumla wa Tuzo ya Usimamizi wa Deni la Serikali katika nchi za Commonwealth of Nations, mafanikio yanayoakisi maboresho makubwa ya mifumo ya usimamizi wa deni yaliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan.
Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa itaendelea kudhibiti gharama za ukopaji, kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuongeza uzalishaji pamoja na mauzo ya nje ili kuendelea kulinda uthabiti wa deni la taifa na uchumi kwa ujumla.

Comments
Post a Comment