Akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27 Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Dkt. Khamis Mussa Omar ametangaza kuwa Serikali inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni 62.33, ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.3 ikilinganishwa na mwaka 2025/26.
Ameeleza kuwa mapato ya Serikali yanakadiriwa kufikia shilingi trilioni 46.79, ambapo mapato ya kodi ni trilioni 36.99, mapato mengine trilioni 9.24 (ikiwemo trilioni 1.97 za Mamlaka za Serikali za Mitaa), huku misaada ya maendeleo ikiwa shilingi bilioni 563.1. Serikali imesisitiza kuwa asilimia 74.2 ya bajeti hiyo itagharamiwa na mapato ya ndani, hatua inayoimarisha uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Aidha, misaada ya maendeleo imepungua kwa asilimia 39.1 kutokana na mabadiliko ya sera za baadhi ya washirika wa maendeleo, ambapo Serikali imewashukuru kwa mchango wao na kusisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji na ulipaji kodi.
Kwa upande wa matumizi, Serikali inakadiriwa kutumia shilingi trilioni 54.50 katika matumizi na uwekezaji (bila kujumuisha malipo ya mtaji wa deni la Serikali).
Kati ya kiasi hicho, mishahara na stahiki za watumishi ni trilioni 10.13, bidhaa na huduma trilioni 5.22, malipo ya riba trilioni 6.86, ruzuku trilioni 25.32, mafao na misaada ya kijamii trilioni 1.01, uwekezaji katika mali zisizo za kifedha trilioni 2.33, na gharama nyingine trilioni 3.63.
Aidha, kutokana na mwenendo wa mapato na matumizi, kunatarajiwa nakisi ya bajeti ya shilingi trilioni 7.71.
Serikali itafadhili pengo hilo kupitia mikopo ya ndani na nje yenye jumla ya shilingi trilioni 15.54, ambapo trilioni 6.56 ni mikopo ya ndani, trilioni 6.55 mikopo nafuu ya nje, na trilioni 2.43 mikopo ya kibiashara. Pia, Serikali inatarajia kulipa deni la mtaji la shilingi trilioni 7.84 kwa mikopo iliyoiva.

Comments
Post a Comment