Serikali imeeleza dhamira yake ya kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku uzalishaji wa ajira ukipewa nafasi ya kipekee katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27.
Akiwasilisha mpango huo bungeni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema mpango huo umeandaliwa kwa lengo la kugeuza maono ya Dira 2050 kuwa miradi na programu zenye matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi, hususan katika kukuza uchumi na kuzalisha ajira.
Mpango wa mwaka 2026/27 ni mwanzo wa utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31), unaobeba dhima ya "Mageuzi kwa Ajili ya Ukuaji Jumuishi wa Uchumi na Uzalishaji Ajira."
Katika kufanikisha lengo hilo, serikali imeelekeza nguvu katika sekta zenye mchango mkubwa wa ajira ikiwemo kilimo, viwanda, madini, utalii, biashara pamoja na huduma za teknolojia na ubunifu, ambazo zinatajwa kuwa nguzo muhimu za kukuza uchumi na kuinua maisha ya wananchi.
Mkazo huo unatarajiwa kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za uzalishaji, kuimarisha kipato cha kaya, kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira na kuhakikisha ukuaji wa uchumi unawanufaisha Watanzania wengi zaidi.
Hatua hiyo pia inaweka msingi wa kuijenga Tanzania yenye uchumi imara, shindani na jumuishi, unaotoa fursa pana za maendeleo kwa vizazi vya sasa na vijavyo kupitia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.



Comments
Post a Comment