AGNES MARWA:NI LINI SERIKALI ITAUPA HADHI UWANJA WA KARUME MUSOMA
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Mhe. Agnes Marwa, ameitaka Serikali kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuuboresha Uwanja wa Karume uliopo Musoma Mjini ili uweze kuwa miongoni mwa viwanja vya kisasa vinavyoweza kutumika kuandaa mashindano makubwa ya kitaifa na kimataifa.
Akiwasilisha swali lake bungeni Leo Jun 17,2026 Bungeni Jijini Dodoma Mhe. Marwa amesema Uwanja wa Karume ni moja ya maeneo yenye historia muhimu katika harakati za ukombozi wa Taifa, akibainisha kuwa viongozi wa harakati za kudai uhuru wa Tanzania walitumia eneo hilo kufanya mikutano iliyoweka msingi wa ukombozi wa nchi.
Amesema licha ya historia na umuhimu wake kwa wananchi wa Mkoa wa Mara, uwanja huo bado haujafikia viwango vinavyoweza kuuwezesha kuwa kitovu cha maendeleo ya michezo na uchumi wa eneo hilo.
Mhe. Marwa alihoji ni lini Serikali itatenga fedha za kuuboresha Uwanja wa Karume ili uweze kuwa mwenyeji wa mechi za ligi mbalimbali, mashindano ya kitaifa na hata michezo ya Timu ya Taifa, hatua itakayosaidia kukuza vipaji vya vijana, kuvutia wageni na kuongeza mapato ya wananchi wa Musoma na Mkoa wa Mara kwa ujumla.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, amesema Serikali ina dhamira ya dhati ya kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya michezo nchini ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa chachu ya maendeleo na ajira kwa vijana.
Ameeleza kuwa kwa sasa Serikali imejielekeza katika kukamilisha miradi ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vinavyotumika kuandaa mashindano ya CHAN na AFCON, ikiwemo Uwanja wa Benjamin Mkapa, Uwanja wa Amaan Zanzibar, viwanja vya Arusha pamoja na viwanja vya mazoezi katika maeneo mbalimbali nchini.
Mhe. Mwinjuma amesema baada ya kukamilika kwa maandalizi ya mashindano hayo, Serikali itaendelea kupanua uwekezaji katika miundombinu ya michezo kwa kuzingatia upatikanaji wa rasilimali fedha, huku maeneo yenye mahitaji makubwa kama Uwanja wa Karume wa Musoma yakipewa nafasi katika mipango ya maendeleo ya sekta hiyo.
Amesisitiza kuwa Serikali inatambua mchango wa michezo katika kukuza uchumi, kuibua vipaji vya vijana na kuimarisha mshikamano wa kitaifa, ndiyo maana itaendelea kuboresha viwanja na miundombinu mingine ya michezo katika maeneo mbalimbali nchini kadri uwezo wa kifedha unavyoruhusu.



Comments
Post a Comment