MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Mhe. Agnes Marwa, ameendelea kuonyesha dhamira yake ya kuwawezesha wananchi kiuchumi baada ya kuwakatia bima ya majanga wajasiriamali wadogo wa mkoa huo kupitia ushirikiano na Benki ya NMB, hatua inayolenga kuwapa kinga dhidi ya athari za majanga mbalimbali yanayoweza kuwakumba katika maisha na shughuli zao za kila siku.
Kupitia bima hiyo, wanufaika watapata msaada wa kifedha endapo watakumbwa na majanga yaliyofunikwa na bima husika, ikiwemo ulemavu wa kudumu, vifo pamoja na matukio mengine yaliyoainishwa kwenye masharti ya bima. Katika baadhi ya matukio, mnufaika anaweza kulipwa hadi Shilingi milioni mbili, fedha zitakazomsaidia kukabiliana na changamoto zinazojitokeza baada ya janga kutokea.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi bima hizo katika Manispaa ya Musoma, Mhe. Marwa amesema lengo la mpango huo ni kuwajengea wajasiriamali wadogo usalama wa kifedha na kuwapa uhakika wa msaada wanapokumbwa na matatizo yanayoweza kuathiri maisha yao na biashara wanazozitegemea.
Amesema kuwa maendeleo ya wananchi hayawezi kutenganishwa na uwepo wa mifumo ya ulinzi wa kijamii, ndiyo maana ameona umuhimu wa kuwafikishia wajasiriamali huduma ya bima ili kuwasaidia kukabiliana na majanga kwa urahisi zaidi.
Kwa upande wao, wanufaika wa bima hiyo walimshukuru na kumpongeza Mhe. Agnes Marwa kwa kuwafikiria na kuwajumuisha katika mpango huo, wakisema ni hatua kubwa inayowapa matumaini mapya na kuondoa hofu ya kukosa msaada wanapopatwa na majanga.
Wamesema bima hiyo itakuwa ngao muhimu kwao na familia zao, hasa katika nyakati ngumu ambazo mara nyingi huathiri uwezo wao wa kuendesha shughuli za kiuchumi.
"Hiki ni kitu kikubwa sana ambacho hakijawahi kufanyika kwa wengi wetu. Tunamshukuru sana Mhe. Agnes Marwa kwa kutuona na kutupa fursa hii muhimu. Bima hii itatupa faraja na msaada mkubwa pale majanga yatakapotokea," amesema mmoja wa wanufaika.
Wanufaika hao wameeleza kuwa hatua hiyo inaonesha namna viongozi wanavyoweza kutumia nafasi zao kuboresha maisha ya wananchi, huku wakitoa rai kwa viongozi wengine kuiga mfano huo kwa kuhamasisha huduma za bima katika jamii.
Mpango huo wa bima ya majanga unatajwa kuwa sehemu ya juhudi za kuwawezesha wajasiriamali wadogo, kuimarisha ustawi wao wa kijamii na kiuchumi, pamoja na kujenga jamii yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazosababishwa na majanga yasiyotegemewa.






Comments
Post a Comment