Klabu ya Young Africans SC (Yanga) sasa ipo huru kufanya usajili wa wachezaji wapya kwa ajili ya mashindano mbalimbali ya ndani na kimataifa, ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya uongozi wa klabu hiyo kuthibitisha kuwa hakuna deni lolote linaloizuia kusajili.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rogers Gumbo, amesema changamoto iliyosababisha klabu kuonekana kwenye orodha ya FIFA ya vilabu vilivyofungiwa usajili ilitokana na kutokamilika kwa baadhi ya taarifa na nyaraka zilizokuwa zinahitajika na FIFA pamoja na CAF, na si deni la kifedha kama ilivyodhaniwa na wengi.
Kwa mujibu wa Gumbo, Mei 31, 2026 ilikuwa siku ya mwisho ya muda wa ziada uliotolewa kwa klabu zilizokuwa na mashauri ya malipo, ambapo Yanga imefanikiwa kutimiza matakwa yote yaliyokuwa yanahitajika.
Awali, kupitia orodha ya FIFA ya vilabu vilivyowekewa zuio la usajili, jina la Yanga lilionekana tangu Mei 3, 2026, jambo lililozua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa soka nchini. Hata hivyo, taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa klabu hiyo imeondoa dosari zote zilizokuwa zimeibuliwa.
Kwa mujibu wa kanuni za utoaji leseni za klabu za Confederation of African Football (CAF), hususan ibara ya 59 hadi 63, klabu zenye madeni au mashauri yasiyokamilika zinaweza kuzuiwa kushiriki mashindano ya kimataifa. Hatua ya Yanga kukamilisha mahitaji yote sasa inaondoa hofu ya kushindwa kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.
“Yanga sasa haina deni la FIFA na ipo tayari kuendelea na mipango yake ya usajili na maandalizi ya mashindano ya kimataifa,” amesema Gumbo.

Comments
Post a Comment