SERIKALI imeendelea kuimarisha vita dhidi ya utakasishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi kwa kutekeleza mageuzi mbalimbali yanayolenga kuimarisha usalama wa mfumo wa fedha nchini na kulinda uchumi wa Taifa.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb),wakati akiwasilisha Bungeni Jijini Dodoma leo Juni 2, 2026, mapitio ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2025/26 pamoja na mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2026/27.
"Tumeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha mifumo ya udhibiti wa fedha haramu ili kuhakikisha sekta ya fedha nchini inakuwa salama, yenye uwazi na inayoendana na viwango vya kimataifa," alisema Waziri Omar.
Amesema hadi Aprili 2026, Wizara kupitia Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu imefanya mapitio na kuhuisha Tathmini ya Taifa ya Vihatarishi ili kuendana na mabadiliko ya mazingira ya kifedha na kukidhi matakwa ya Kikosi Kazi cha Kimataifa cha Kudhibiti Utakasishaji Fedha Haramu (FATF).
Katika hatua nyingine, Serikali imeandaa na kusambaza mwongozo maalum wa utekelezaji wa sheria za kupambana na utakasishaji wa fedha haramu, hatua inayolenga kuongeza uelewa na ufanisi wa wadau katika kutekeleza wajibu wao wa kisheria.
"Mapambano dhidi ya fedha haramu yanahitaji ushirikiano mpana wa wadau wote. Ndiyo maana tumeendelea kutoa elimu na mafunzo ili kuongeza uwezo wa taasisi mbalimbali kutambua na kudhibiti vihatarishi vinavyojitokeza," Amesisitiza.
Waziri Omar amebainisha kuwa jumla ya wadau 3,338 wamepatiwa elimu kuhusu wajibu wa kusimamia na kudhibiti utakasishaji wa fedha haramu, huku asasi 800 zikifundishwa kuhusu masuala ya ufadhili wa ugaidi na mbinu za kutambua vihatarishi katika shughuli zao.
Aidha, Serikali imeboresha Mfumo wa Taifa wa Takwimu za Utakasishaji Fedha Haramu (NASMS) na kuuunganisha na mifumo ya Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) pamoja na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), hatua inayoongeza ufanisi wa ukusanyaji, uchambuzi na matumizi ya taarifa katika kukabiliana na uhalifu wa kifedha.
Katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, Tanzania pia ilifanikiwa kuratibu Mkutano wa Kimataifa wa Vitengo vya Kudhibiti Fedha Haramu Duniani (Egmont Group of FIUs) uliofanyika Jijini Arusha Januari 26 hadi 30, 2026, ukileta pamoja wataalamu na wadau kutoka mataifa mbalimbali kujadili mikakati ya kisasa ya kukabiliana na uhalifu wa kifedha.
Hatua hizo zinaakisi dhamira thabiti ya Serikali ya kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa na mfumo wa fedha ulio salama, unaoaminika na unaokidhi viwango vya kimataifa, huku ikilinda maslahi ya Taifa dhidi ya vitendo vya utakatishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi.





Comments
Post a Comment