RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameanza rasmi ziara yake ya kiserikali nchini Urusi kwa kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu na mwenyeji wake, Vladimir Putin, katika Ikulu ya Kremlin jijini Moscow.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Urusi katika sekta mbalimbali za kimkakati zenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Rais Dkt. Samia amesema ziara hiyo ni ya kihistoria na inaashiria mwanzo wa hatua mpya ya ushirikiano wenye tija kwa wananchi wa mataifa hayo mawili. Amesema Tanzania inaendelea kuona fursa kubwa za ushirikiano katika sekta ya kilimo, hususan uzalishaji wa mbolea, kilimo cha biashara na uongezaji thamani wa mazao ili kuongeza uzalishaji, ajira na ukuaji wa uchumi.
Viongozi hao pia walijadili maeneo ya teknolojia za kidijitali, serikali mtandao, akili bandia (AI), sayansi ya anga na mafunzo ya teknolojia za kisasa kwa vijana na wataalamu wa Tanzania, hatua inayolenga kuharakisha mageuzi ya kidijitali na kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa.
Katika sekta ya nishati, marais hao walisisitiza umuhimu wa kupanua vyanzo vya nishati vya uhakika vitakavyochochea ukuaji wa viwanda, uwekezaji na maendeleo ya uchumi, sambamba na kuangalia fursa za matumizi ya teknolojia za kisasa katika uzalishaji wa nishati.
Aidha, Rais Dkt. Samia amesisitiza kuimarishwa kwa ushirikiano katika sekta ya afya, ikiwemo uzalishaji wa dawa, chanjo na bidhaa nyingine za afya pamoja na kujenga uwezo wa wataalamu ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Katika eneo la elimu, viongozi hao walikubaliana kuongeza fursa za mafunzo, ufadhili wa masomo, kubadilishana utaalamu na kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma katika sayansi, teknolojia, uhandisi na taaluma nyingine za kimkakati kwa ajili ya kuandaa rasilimali watu yenye ushindani katika soko la dunia.
"Tanzania na Urusi zina dhamira ya kuendeleza ushirikiano wa kimkakati unaolenga maendeleo endelevu, uhamishaji wa teknolojia na ustawi wa wananchi wa mataifa yote mawili."






Comments
Post a Comment