Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Charles Mahera, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuleta mapinduzi makubwa katika sekta za elimu na afya kupitia uwekezaji wa mabilioni ya shilingi unaolenga kuboresha huduma za kijamii na kuinua maisha ya wananchi.
Akizungumza leo Jun 3,2026 katika Viwanja Jijini Dodoma,Dkt. Mahera amesema katika sekta ya elimu, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya vyuo vya VETA nchini kwa kujenga na kuendeleza vyuo katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma hiyo, sambamba na kusambaza vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia ili kuongeza ufanisi wa mafunzo kwa vijana.
Ameeleza kuwa Jimbo la Butiama limeendelea kunufaika na fedha za maendeleo zilizotolewa na Serikali, ambapo zaidi ya shilingi milioni 524 zimeelekezwa katika kuboresha miundombinu ya shule mbalimbali ikiwemo ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu na mazingira bora ya kujifunzia.
"Leo tunashuhudia matokeo ya dhamira ya Rais Samia katika kuwekeza kwenye elimu. Shule ambazo zilikuwa na changamoto kubwa za miundombinu sasa zinapata fedha za ukarabati na ujenzi wa madarasa mapya, jambo litakaloongeza ubora wa elimu kwa watoto wetu," amesema Dkt. Mahera.
Amesema Shule za Msingi Buswahili na Nyakisura zimepokea zaidi ya shilingi milioni 125 kwa ajili ya kuboresha miundombinu, huku Kijiji cha Nyarukoro kilichopo Kata ya Bisumwa kikinufaika na shilingi milioni 75 za ujenzi wa madarasa mapya.
Aidha, Shule ya Msingi Buswahili imepata shilingi milioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu, hatua inayotarajiwa kuongeza motisha na kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu.
Katika sekta ya afya, Dkt. Mahera amesema Serikali imeendelea kuimarisha huduma za matibabu kwa kutenga fedha kwa ajili ya vifaa tiba na maboresho ya vituo vya afya, ambapo Kituo cha Afya Kukilango kimepokea shilingi milioni 120 kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa vifaa na huduma muhimu za afya.
"Fedha hizi zinaonyesha namna Serikali ya Rais Samia ilivyojipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za elimu na afya karibu na maeneo yao. Huu ni uwekezaji unaokwenda kugusa maisha ya watu moja kwa moja," amesema.
Mbunge huyo ameongeza kuwa maendeleo yanayoendelea kushuhudiwa Butiama ni matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali na wananchi, huku akiahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi yote ili kuhakikisha fedha zinazotolewa zinaleta matokeo yaliyokusudiwa.
"Butiama ya leo inaendelea kupiga hatua kwa kasi kupitia uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika elimu, afya na huduma nyingine za maendeleo." — Dkt. Charles Mahera, Mbunge wa Jimbo la Butiama.

Comments
Post a Comment