Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Charles Mahera, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya miundombinu ya barabara na madaraja, akisema hatua hiyo inaendelea kubadilisha maisha ya wananchi na kufungua fursa mpya za kiuchumi katika jimbo hilo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Viwanja vya Bunge leo Jun 3,2026, Dkt. Mahera amesema Jimbo la Butiama limetengewa shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa barabara za kiwango cha changarawe pamoja na madaraja yaliyoathiriwa na mafuriko, huku zaidi ya shilingi bilioni 2.5 zikielekezwa katika miradi ya TARURA.
Amesema uwekezaji huo unaashiria dhamira ya dhati ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata miundombinu bora inayorahisisha usafiri, usafirishaji wa mazao na upatikanaji wa huduma za kijamii.
"Bajeti hii imeleta matumaini makubwa kwa wananchi wa Butiama. Barabara nyingi ambazo zilikuwa ndoto kwa muda mrefu sasa zinaenda kutekelezwa na kufungua fursa mpya za maendeleo," amesema Dkt. Mahera.
Mbunge huyo ameeleza kuwa miongoni mwa miradi itakayoanza kutekelezwa ni barabara ya Nyambiri–Nyandewa–Buswahili, ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu na wananchi wa Kata ya Buswahili.
Dkt. Mahera pia ameipongeza Serikali kwa kukamilisha Daraja la Mang'atika, mradi uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu kutokana na umuhimu wake katika kuunganisha wananchi na kurahisisha shughuli za kiuchumi.
Amesema pamoja na daraja hilo, Serikali imefanikiwa kuboresha na kukamilisha madaraja mengine muhimu ambayo itafungua mawasiliano katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji.
"Kila tunapoidhinisha bajeti hapa Bungeni, wananchi wanahitaji kuona matokeo yake kwa vitendo. Leo Butiama inaendelea kushuhudia matokeo hayo kupitia madaraja yanayokamilika na barabara zinazoendelea kujengwa," amesema Dkt. Mahera.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utaongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi, kuboresha huduma za kijamii na kuimarisha mawasiliano kati ya vijiji, kata na maeneo mengine ya jimbo hilo.
"Kwa kweli bajeti hii na utekelezaji wake ni ushahidi wa namna Serikali inavyoendelea kuwagusa wananchi moja kwa moja kupitia uwekezaji mkubwa wa miundombinu. Butiama inaendelea kufunguka na kusonga mbele," amesisitiza Dkt. Mahera.

Comments
Post a Comment