Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 358.36 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema wizara hiyo pia inatarajia kukusanya maduhuli ya Serikali yenye thamani ya shilingi bilioni 1.511 kutoka katika vyanzo mbalimbali vinavyosimamiwa na makao makuu ya wizara pamoja na balozi za Tanzania zilizopo nje ya nchi.
Amefafanua kuwa vyanzo hivyo vya mapato ni pamoja na upangishaji wa nyumba za Serikali zilizopo nje ya nchi, upangishaji wa kumbi za mikutano pamoja na huduma za uthibitishaji wa nyaraka mbalimbali kama vyeti vya elimu, vyeti vya ndoa, hati za talaka na nyaraka nyingine rasmi.
Kwa mujibu wa makadirio hayo, wizara imepanga kutumia jumla ya shilingi bilioni 358.36, ambapo kati ya hizo shilingi bilioni 312 zitaelekezwa katika matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 46.36 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Aidha, kati ya fedha za matumizi ya kawaida, shilingi bilioni 290.299 zimetengwa kwa matumizi mengineyo, huku shilingi bilioni 22.66 zikielekezwa katika mishahara ya watumishi wa wizara makao makuu na balozi za Tanzania zilizopo nje ya nchi, hatua inayoonesha dhamira ya kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya diplomasia ya Taifa.

Comments
Post a Comment