Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini mkoani Mara, Esther Bulaya amesema Tanzania ni nchi huru na haiwezi kuingiliwa na mataifa mengine, huku akisisitiza kuwa ushirikiano wa kimataifa lazima uzingatie maslahi ya Taifa.
Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki bungeni jijini Dodoma, Bulaya amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha diplomasia ya kimataifa na kuimarisha mahusiano na mataifa mbalimbali duniani.
Amesema hatua hiyo imeongeza heshima na ushawishi wa Tanzania katika jukwaa la kimataifa, pamoja na kuleta manufaa katika sekta za uchumi, ulinzi na maendeleo ya kijamii.
Aidha, Bulaya amesisitiza kuwa licha ya Tanzania kunufaika na ushirikiano wa kimataifa, Serikali ina wajibu wa kulinda haki na maslahi ya Watanzania wakati wote.
Ameeleza kuwa kuwa Tanzania itaendelea kuwa mshirika mwema wa mataifa mengine, lakini itaweka mbele maslahi ya Taifa katika kila hatua ya ushirikiano wa kimataifa.
Bulaya amesema kuwa Tanzania na Marekani zina mahusiano ya kidiplomasia ya muda mrefu ambayo yanapaswa kulindwa kwa manufaa ya pande zote mbili, lakini akasisitiza kuwa hayo hayapaswi kutumika kama kisingizio cha kuingilia mambo ya ndani ya nchi.
Amesema kwa mujibu wa Katiba na sheria za Tanzania, nchi ina uwezo wa kushughulikia masuala yake ya ndani kwa mujibu wa taratibu zake bila shinikizo la nje.
Aidha, ametoa wito kwa watu wote wanaojaribu kudhoofisha au kuvunja heshima ya mamlaka kamili ya taifa kuacha kutumia visingizio vya kidiplomasia kujinufaisha binafsi au kisiasa.

Comments
Post a Comment