WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema Serikali imejipanga kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya usafiri wa majini baada ya kutenga Shilingi bilioni 171 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya, ukarabati wa meli kongwe na utekelezaji wa miradi mikubwa kupitia Tanzania Shipping Company Limited (TASHICO).
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi leo Mei 13, 2026 Bungeni jijini Dodoma, Prof. Mbarawa amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha uchumi wa buluu, kuongeza usalama wa usafiri wa majini na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya usafiri wa maji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Katika mpango huo, Serikali itajenga meli mpya ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3,500 katika Ziwa Tanganyika, sambamba na kuanza ujenzi wa meli mbili za mafuta zenye uwezo wa kubeba lita 600,000 kila moja.
Pia, Serikali itajenga meli mpya ya abiria yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo katika ziwa hilo, hatua inayotarajiwa kuongeza kasi ya usafirishaji wa watu na bidhaa katika maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika.
Katika Ziwa Victoria, Serikali imepanga kujenga meli mpya ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 huku ikiendelea na ukarabati mkubwa wa meli za MT. Nyangumi na MV. Clarias ili kuboresha huduma za usafiri na biashara.
“Miradi hii ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kufungua fursa mpya za kiuchumi kupitia usafiri wa majini na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa Taifa,” amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, Serikali itakamilisha upembuzi yakinifu wa kuiwezesha TASHICO kufanya biashara katika Bahari ya Hindi, pamoja na kujenga kiwanda cha kisasa cha kujengea meli katika Ziwa Tanganyika chenye uwezo wa kuhudumia meli zenye uzito wa hadi tani 5,000.
Serikali pia itaendelea na ukarabati wa meli ya MV. Mwongozo na MV. Liemba katika Ziwa Tanganyika, kufanya ukarabati wa meli ya MV. Songea katika Ziwa Nyasa, kununua mabehewa ya kubeba mizigo kwa ajili ya MV. Umoja pamoja na boti za uokoaji katika maziwa makuu nchini.
Prof. Mbarawa amesema utekelezaji wa miradi hiyo utaongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na abiria, kuimarisha usalama wa safari za majini, kuchochea biashara za ndani na nje ya nchi pamoja na kuongeza ajira na fursa za uwekezaji kwa Watanzania.






Comments
Post a Comment