DODOMA.
KATIKA kuchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini, Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) imesema Mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi asilia kutoka Dar es Salaam Hadi Chalinze umeanza kutekelezwa.
Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza Januari 2027 na kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 15 hadi kukamilika kwake.
Akieleza Mafanikio yaliyopatikana katika siku 100 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Leo jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mussa Makame amsesema Utekelezaji wa mradi huo umeshaanza
Amesema hadi Sasa mkuza kutoka Kinyerezi hadi Chalinze umepatikana na tathmini ya hali ya udongo kwa eneo lote la mkuza ipo hatua za mwisho kukamilika.
"Upembuzi yakinifu wa mradi (feasibility study) inaendelea na Ujenzi wa mradi unatarajiwa kuanza Januari 2027 na kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 15 hadi kukamilika kwake". Amesema
"Mradi huu ukikamilika utafungua fursa mpya za uwekezaji wa viwanda na hivyo kuchochea ajira kwa vijana katika ukanda huo, sambamba na kuongeza wigo wa wateja wa gesi asilia". Amesisitiza
Sambamba na Hayo, Mkurugenzi huyo amesema serikali inaendelea na usambazaji wa Gesi asilia kwa Matumizi ya viwandani, majumbani, kwenye taasisi na kwenye vyombo vya usafiri.
"Tunaendelea na kupanua miundombinu ya kusambaza gesi gesi asilia kwa matumizi ya viwandani na majumbani katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara na sasa mpango ni kufika Morogoro, Dodoma, Tanga, Kilimanjaro na Arusha". Amesema
Sambamba na hilo, amesema, Shirika kwa kushirikiana na sekta binafsi linaendelea na ujenzi wa vituo vya kujaza gesi asilia kwenye magari (CNG-V Stations) pamoja na ununuzi na uendeshaji wa vituo vya CNG vinavyohamishika (CNG-V Mobile Stations) kwa ajili ya kuhudumia magari na vyombo vingine vya moto katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
"Hadi sasa jumla ya vituo 14 vimekamilika na vinatoa huduma kwa vyombo mbalimbali vya usafiri vikiwemo magari madogo na makubwa, bajaji na mabasi ya mwendokasi". Amesema
"Lengo la ujenzi wa vituo hivi ni kuhamasisha matumizi ya gesi asilia katika sekta ya usafirishaji, kupunguza utegemezi wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi, kupunguza gharama za uendeshaji wa vyombo vya moto na kuchangia katika kupunguza hewa ukaa na athari za mabadiliko ya tabianchi". Amesisitiza
Katika mwaka wa fedha 2025/2026, TPDC inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo Miradi hii inalenga kuongeza upatikanaji wa gesi asilia, kupanua wigo wa usambazaji wa mafuta na gesi asilia na kuzingatia utekelezaji wa miradi ya CSR na ushirikishwaji wa wazawa katika mnyororo wa thamani wa sekta ya mafuta na gesi.






