Waziri Kombo Akutana na Katibu Mkuu wa Imo Kuimarisha Ushirikiano wa Masuala ya Bahari

GEORGE MARATO TV
0


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo amekutana kwa mazungumzo na Katibu Mkuu wa Shirika la Bahari Duniani (IMO), Bw. Arsenio Domínguez, jijini London.

Mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na IMO hususan katika nyanja za usalama wa baharini, ulinzi, utunzaji wa mazingira ya bahari na kujengeana uwezo.

Mhe. Waziri Kombo alieleza jinsi Serikali ya Tanzania inavyothamini ushirikiano na IMO na mchango wake katika kuimarisha nafasi ya Tanzania kama taifa muhimu katika eneo la Bahari ya Hindi, akisisitiza nafasi ya Tanzania katika jitihada za utunzaji wa rasilimali bahari ili iendelee kuwa na mchango kwenye uchumi ikiwemo kupitia bandari ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika biashara ya kikanda na ya kimataifa.

“Tunaitambua IMO kama mshirika muhimu katika kujenga uwezo wa Tanzania kwenye masuala ya bahari na kusaidia juhudi zetu za kuboresha sekta hii kwa kuzingatia viwango vya kimataifa,” alisema Mhe. Waziri Kombo.

Naye  Katibu Mkuu wa IMO Domínguez aliipongeza Tanzania kwa ushiriki wake wa dhati katika programu na miradi ya IMO na kuahidi kuendelea kushirikiana katika maeneo ya mafunzo, fursa za ajira, utawala wa masuala ya bahari, mchakato wa kupunguza hewa ukaa kwenye usafiri wa meli, na mapambano dhidi ya uvuvi haramu, usioripotiwa na usiodhibitiwa (IUU).

“Tanzania ni mshirika muhimu wa masuala ya bahari, na tumejipanga kushirikiana kwa karibu na Serikali kuhakikisha sekta ya bandari na usafirishaji inaendelea kukua kwa njia endelevu sambamba na kanuni za kimataifa za usalama na mazingira,” alisema.

Mazungumzo hayo pia yaligusia fursa za kuimarisha msaada wa kiufundi kwa mabaharia wa Kitanzania, kuongeza uwezo wa taasisi za masuala ya bahari, na kulinganisha mkakati wa Tanzania wa Uchumi wa Buluu na ajenda ya IMO ya mabadiliko ya kijani na kidijitali katika sekta ya usafirishaji majini.

Waziri Kombo yuko nchini Uingereza kwa ziara rasmi ambayo pamoja na masuala mengine inalenga kuendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria na kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Uingereza.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top