Na MASHAKA MHANDO, Tanga
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha National League for Democracy (NLD) Zanzibar Ahmed Salim Hamad amesema wanamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa magari wagombea wa vyama vingine ili wajinadi katika kampeni zinazoendela kabla ya uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za chama hicho zilizofanyika kwenye uwanja wa Komesho Jijini Tanga, Leo Septemba 4 Hamad alisema kitendo kilichofanywa na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi ni kitendo cha kuimarisha demokrasia nchini ukomavu wa kisiasa.
Alisema Rais Dkt Samia kwa kitendo hicho ameonesha kwamba anakwenda kufanya uchaguzi wa haki na usawa kwa wagombea wote na chama hicho kinampongeza kwa uwamuzi huo.
"Mama yetu mama Samia (Dkt Samia Suluhu Hassan) amekusudia kufanya uchaguzi wa haki, nampongeza sana, haijawahi kutokea mgombea unashindaba naye kutaka nafasi yake halafu anakupa gari linalofanana na analopanda yeye, huku ni kuinarisha demokrasia nchini," alisema Hamad.
Hamad ambaye pia anagombea ubunge jimbo la Wingwi wilaya ya Micheweni, alisema kuwa Chama chao kitaendesha kampeni za kistaarabu ili kuomba kura kwa Watanzania.
Akizungumaka katika uzinduzi huo Mgombea Urais kupitia Chama hicho Doyo Hassan Doyo ametangaza vipaumbele sita watakavyoanza navyo endapo watashinda Urais.
Alisema kwenye ilani ya Chama chao wameandaa dira itakayokuwa na vipaumbele hivyo ambayo ni pamoja na kujenga Tanzania yenye kujumuisha rasilimali za Taifa.
Alisema ili kufanikisha dira hiyo itaongizwa na misingi ya uzalendo, haki, usawa, uwajibikaji, uwezeshaji na kuongeza thamani rasilimali za Taifa.
Pia alisema watajenga taasisi imara zenye kusimamia haki na uwajibikaji katika kuwahudumia wananchi katika sekta za umma.
Pia alisema chama hicho endapo kitachaguliwa kitafuta mishahara mkubwa ya wabunge na kuweka mshahara wa shilingi milioni 1.5 na kuwalipa wataalamu shilingi milioni 12.
Pia mgombea huyo ambaye alisema amezindua kampeni nyumbani kwao Tanga ili kupata Baraka za wazee alisema kuwa atahakikisha viongozi wanawajibika ipasavyo na wanakuwa na maadili ya uongozi.






