Miaka mitano ijayo wananchi Muheza mtakuwa na maji majumbani- MwanaFA

GEORGE MARATO TV
0


Na Mwandishi Wetu, Muheza

MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Muheza kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hamisi Mwinjuma maarufu MwanaFA amesema endapo atachaguliwa kuwa mbunge wananchi wa kata ya Lusanga na Muheza kwa ujumla wataweka maji ya bomba nyumbani kwao badala ya kuchota kwenye vilula.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni katika kata ya Lusanga, MwanaFA alisema kuwa tatizo la maji Muheza kabla hajakuwa mbunge, wilaya hiyo ilikuwa na shida ya maji kubwa lakini Sasa kuna ahueni ya kutosha.

Alisema kata ya Lusanga pekee ilipata kiasi cha shilingi milioni 700 kwa ajili ya miradi ya maji ambayo ilipunguza tatizo hilo kwa wananchi.

Aliwahakikishia wananchi hao kwamba fedha zaidi za maji zitakuja wilayani humo kupitia mradi wa Green Bond ambao umechangiwa kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya miradi ya maji mkoa wa Tanga na Muheza utashughulikia kiasi cha kilomita 15 ili maji yawe majumbani.

"Tunataka ndani ya miaka mitano ijayo sehemu ya Lusanga Kila mtu ameweka maji nyumbani kwake na asiende kuchota kwenye kilula," alisema.

Alisema amefika kwenye mkutano huo kuomba kura ili pamoja na viongozi wenzake wachaguliwe ili wamalizie Yale walioanza katika miaka mitano inayoisha.

Akizungumza miradi mbalimbali iliyotekelezwa katika kata hiyo alisema jumla ya shilingi bilioni 3.5 zililetwa katika kata hiyo kwa ajili ya ujenzi wa hospital ya wilaya ambayo Sasa inafanya kazi.

Alisema pia shilingi bilioni 3 zimeletwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya wilaya Muheza ambalo linaendelea kujengwa katika kata hiyo.

Pia katika sekta ya Elimu kiasi cha shilingi milioni 300 kimeletwa kwa ajili ya kushughulikia kukarabati na kujenga Majengo ya Elimu ya sekondari na msingi katika kata hiyo.

MwanaFA ambaye ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alisema kuhusu Umeme vitongoji 18 kati ya 19 vyote vimepata Umeme kasoro kimoja cha Kweusanga ambacho nacho ameaahidi kitapata Umeme ili wananchi wafurahie Nishati hiyo.

Alisema kuhusu mikopo ya vikundi vya akina mama, vijana na watu wenye mahitaji maalum, wilaya imekuwa ikizitenga kama takwa la kisheria ambapo katika kipindi cha nyuma wilaya hiyo ilitoa kiasi cha shilingi milioni Tano tu.

Alisema mwaka jana wameweza kutoa kiasi cha shilingi milioni 730 kwa vikundi mbalimbali vya makundi hayo.

Hivyo mgombea huyo aliwahakikishia wananchi kwamba wataendele kupata mikopo hiyo na akawasihi vikundi vingine vilivyopata wafanye marejesho ili wenzao nao wapate.

Akizungumza hali ya Elimu kwa ujumla katika Jimbo hilo alisema wameweza kujenga vyumba 390 vya madarasa, shule mpya 11 zimejengwa na kulikuwa na kata 13 hazina shule za sekondari lakini Sasa zimebaki kata mbili tu. 

"Suala la maendeleo ndugu zangu ni mchakato sisi kama viongozi wenu mkitupa  dhamana tutaendelea kushughulika nayo kadiri tunapopata nafasi," alisema.

Kuhusu afya alisema kwamba wilaya ya Muheza tangu ianzishwe mwaka 1974 ilikuwa na kituo cha afya kimoja na kwamba alipoingia madarakani amewezesha kujengwa vituo vya afya vitatu.

Aliwaahidi wananchi kwamba ilani ya CCM ya mwaka 2025-2030 inakwenda kufanya mambo makubwa nchini ikiwemo Muheza hivyo amewaahidi wananchi waendelee kuwa na imani na CCM na viongozi wake kwakuwa ndiyo chama pekee nchini kitakacholeta maendeleo katika nchi hii.

MwanaFA aliwaomba wananchi wamchague Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kumpa kura nyingi tofauti na maeneo mengine lakini pia wamchague yeye awe mbunge wa Muheza pamoja na diwania Anthony Kabula wa kata ya Lusanga.

Aliwata wananchi wa Muheza waachane na wagombea wa upinzani ambao kiujumla vyama vyao wamevifanya kama miradi ya vikoba hivyo amewataka wananchi waachane navyo.











 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top