Na Ada Ouko GMTV, Musoma.
JESHI la Magereza mkoa wa Mara limeadhimisha miaka 64 ya kuasisiwa kwake kwa kushiriki matendo ya huruma kwa jamii, ikiwa ni pamoja na kufanya usafi wa mazingira katika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kata ya Kwangwa Manispaa ya Musoma.
Kamishina msaidizi wa jeshi hilo, Mkuu wa magereza mkoani humo Hospitius Mendi amesema maadhimisho hayo yamezinduliwa leo Agosti 23,2025 nchini kote na kwamba kilele chake kitafanyika Agosti 26,2025 lengo likiwa ni kutoa elimu kwa jamii juu ya shughuli zingine zinazotolewa na jeshi hilo tofauti na kurekebisha maadili kwa wafungwa.
" Tunaenda maeneo kama hayo ili jamii iweze kutambua kuwa jeshi la Magereza hatufanyi tu kazi ya kuwachunga wafungwa pekee yake lakini ni pamoja na kushirikiana na jamii kwenye maendeleo na kuhifadhi mazingira katika hali ya usafi na usalama wa wananchi kwa ujumla" alisema Mendi.
Amesema kauli mbiu ya maadhimisho hayo inasema"Ushirikiano wa Jeshi la Magereza na Jamii kwa urekebishaji wenye tija" na kutoa wito kwa jamii kushirikiana kwa pamoja na jeshi hilo katika kuwarekebisha wahalifu sambamba na hilo kuondoa dhana ya mfungwa amelaaniwa.
" Kila mmoja anaweza kuwa mfungwa isipokuwa wale wanaoenda kinyume na sheria, kanuni na taratibu za nchi, hao wanakuwa watuhumiwa na Mahakama inafanya sehemu yake wanahukumiwa na ndipo wanakuja hapa ndani magereza kwa ajili ya kurekebishwa ili pale wanapokuwa sawa warudi kwenye jamii tunaomba jamii isiwanyanyapae" Aliongeza kusema.
Kamishina Mendi amesema jamii inapaswa kuwapokea wafungwa kwa mtazamo chanya punde, wanapokuwa wamemaliza kutumikia vifungo vyao kama raia wema kwa kuwa muda wote wanapokuwa gerezani wanarekebishwa tabia na baadhi yao hupata mafunzo mbalimbali yakiwemo ufundi ujenzi, ushonaji, udereva, useremala na wengine wanasomea.
Aidha, amesema miongoni mwa shughuli watakazozitekeleza katika maadhimisho hayo ni pamoja na kuchangia damu salama katika benki ya damu salama,kuwatembelea makundi ya watu wenye uhitaji kama vile yatima, wazee, wagonjwa na kuwafikia wasichana wanaoishi kwenye nyumba salama( watoto wa kike waliokimbia familia zao kuepuka kufanyiwa vitendo vya ukeketaji).
Awali Afisa Urekebu Magereza mkoani hapa Veronica Kazimili alisema urekebu ni mchakato wa kumrekebisha mfungwa kwa njia ya nidhamu, elimu, mafunzo ya kaI, dini na ushauri nasaha ili kubadili tambia na kumuandaa kurudi katika jamii akiwa raia mwema.
" Dhana kuu ni kumrekebisha na kumjenga mfungwa upya kimaadili, kisaikolojia, na kijamii badala ya kumwadhibu pekee, kwa lengo la kuhakikisha anajumuika kwenye jamii bila kurudia makosa
Veronica amesema changamoto zinazokabili utekelezaji wa huduma ya urekebishaji wafungwa magerezani ni upungufu wa rasilimali, msongamano wa wafungwa magerezani, mtazamo hasi wa jamii dhidi ya wafungwa na ukosefu wa wataalamu wa ushauri nasaha.
Kwa upande wake Afisa ustawi wa jamii Hospitali hiyo ya Rufaa mkoani humo Paul Nesphory ametoa shukurani kwa niaba ya Mganga Mfawidhi ya Hospitali hiyo alisema kwa kitendo walichofanya jeshi hilo kimesababisha taasisi hiyo ya kiafya kuonekana safi na yenye mazingira ya kuvutia.
" Wametubariki kwa walivyofika na kufanya usafi kwenye taasisi yetu, wameshiriki katika nyanja mbalimbali pia mara kadhaa wamekuwa wakituletea namba ya wafungwa kwa ajili ya kusafisha mazingira ya hospitali, Bado hospitali yetu inahitaji kwa jamii kuja kutushika mkono katika uchangiaji wa damu,msaada kwa wagonjwa kutoka kwa wasamaria wema kwa ujumla tunafungua milango kwa taasisi zote kuja kutushika mkono" alisema Paul.












