Jumuiya ya Ulaya yaipa Veta Bilioni 190 Kuhudumia Vijana

GEORGE MARATO TV
0


Na Mwandishi Wetu Tanga

MKUU wa mkoa wa Tanga, Balozi Dkt Batlida Salha Burian, amekitaka Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) watakaosimamia mradi wa vijana wa (IncluCities) kuhakikisha wanapata vijana watakaokuwa tayari kujifunza na kuuheshimisha mradi huo.

Aidha, alisema pamoja na hilo pia wachague vijana kutoka familia masikini ambao watakapojifunza na kufanya kazi watanufaisha familia zao mara baada ya kumaliza mafunzo ambayo yatamuwezesha kuondoka na zana zake za kazi.

Akizungumza jana wakati alizindua mradi huo wa IncluCities, Mkuu wa mkoa alisema ni vema VETA wabuni mafunzo ambayo yatamuwezesha kijana akimaliza mafunzo hayo anakwenda moja kwa moja kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.

"Vijana 350 watakaopata mafunzo ya mradi huu hakikisheni ni wale watakaojifunza kweli, lakini pia tazameni wale wanaotoka familia masikini ili wakimaliza waweze kuzisaidia familia zao kiuchumi," alisema Balozi Dkt Batlida.

Alisema nchi zilizoendelea mfano China na Vietnam watoto wao wanajifunza Stadi za maisha wakiwa shule za awali ambazo zinawawezesha kujua mambo mbalimbali na anapo maliza hutafuta kozi nyingine kwa ajili ya utaalamu.

Alisema nchini kwetu zipo fursa nyingi lakini vijana wanashindwa kuzitumia akatoa mfano katika misitu asili iliyopo Lushoto na Amani Muheza, vijana wetu wanaweza kwenda kuchuma matunda au uyoga na kuuza kupata mtaji utakaomwezesha kuanza biashara ya kufuga kuku bila kuomba mtaji kokote lakini wanashindwa kufanya hivyo.

Alisema Veta lazima watilie mkazo mafunzo ambayo kijana anapoyapata yanamwezesha kufanya kazi ya kujiajiri na asikae kusubiri ajira serikalini.

Veta mkoani Tanga imepokea fedha kiasi cha shilingi Billion 190, kwa ajili ya  kukamilisha mradi wa (INCLUCITIES) ulioko chini ya Programu ya SASA kwa kishirikiana na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ubelgiji (ENABEL), kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya.

Mkuu wa Chuo cha VETA mkoani Tanga Gideon Ole Lairumbe alisema mradi huo utakaotekelezwa utawagusa na kuwanufaisha vijana 350 wakiwemo wanawake kwa asilimia 50, katika jiji la Tanga ambapo kutakuwa na Programu kuu tatu.

Lairumbe alisema programu ya kwanza ni kuwaandaa na kuwajengea uwezo wa kujiajiri au kuajirika vijana 150, kuwapa ujuzi vijana 150 walioko sokoni, pamoja na utambuzi wa ujuzi  uliopatikana nje ya mfumo usiyo rasmi ambao utagusa vijana 50.

Alisema lengo kuu la mradi huo ni kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi ili kuzalisha wahitimu wanaohitajika katika soko la ajira na kufanya VETA Tanga kuwa kituo cha umahiri wa utoaji mafunzo kwenye sekta husika ili waweze kujiajiri au kuajiriwa baada ya kukamilisha mafunzo yao.

"Tunaamini kwa elimu ya vitendo na ushirikiano kati ya waajiri na wadau mbalimbali wa maendeleo itasaidia kuelekea kupunguza ukosefu wa ajiri na kuongezea kipato kwa wahitimu wetu, 

"Tunategemea kuwa baada ya mafunzo haya, zaidi ya asilimia 75 ya wahitimu watakaopata ujuzi watakuwa katika nafasi nzuri ya kuingia sokoni kwa kujiamini zaidi" alifafanua Lairumbe.

Naye Mshauri Mtaalamu wa ENABEL, Thomas Aikaruwa alisema VETA Tanga imefanya jambo jema kuamua kuboresha chuo hicho kuwa na umahiri kwenye maeneo kama, uchomeleaji, usindikaji chakula, umeme jua na uvuvi.

Alibainisha kwamba Umoja wa Ulaya kupitia Programu yake ya SASA inafanya shuhuli zake kwa kushirikiana na serikali nchini kwenye sekta hizo ili kuchangia katika Mikoa ya Tanga, Mwanza na Pemba kwa upande wa Visiwani.

"Lengo kuu la Programu hii ni kusaidia kuboresha maisha ya Mtanzania wa kawaida kwenye njia tatu, moja ni miundombinu inayozingatia mabadiliko ya tabianchi, kuongezea ukuaji wa uchumi lakini pia kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wa Mikoa hiyo,

"Katika ukuaji wa uchumi, kwa mwananchi huyu wa kawaida, mradi wa INCLUCITIES chini ya Shirika la Ubelgiji (ENABEL) unafanya kazi kwa karibu na uwezo wake na wadau muhimu kwenye sekta hii ya kukuza ujuzi, hasa wadau ambao wanafanya shughuli zao kwenye maeneo haya" alisema.

Hata hivyo Aikaruwa alibainisha kwamba muda wa maandalizi ya mradi huo ulianza mwaka 2022 na unategemewa kwenda hadi mwaka 2027.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top