Skip to main content

@marato_tv

@marato_tv
#sauti_ya_jamii

Tija kwa Nchi ndiyo kipaumbele cha utekelezaji wa mradi wa kuchakata gesi asilia ( LNG ) - DKT Biteko

 

📌 *Asema kiu ya Serikali ni kuona mradi unatekelezwa ila maslahi ya Taifa ndiyo kipaumbele*

📌 *Alieleza Bunge hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhamasisha ujenzi wa vituo vya gesi (CNG) na matumizi*

📌 *Aeleza kuhusu kuundwa kwa Timu kuangalia unafuu wa gharama za umeme kwa Wananchi*

📌 *Kapinga azungumzia kazi za kupeleka umeme wa Gridi Rukwa, Kagera, Katavi, Lindi na Mtwara*

📌 *Shilingi Bilioni 9.89 kupeleka umeme jua kwenye visiwa 118*

📌 *Bunge lapitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati 2025/2026 kwa asilimia 100*

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko amesema dhamira ya Serikali ni kutekeleza mradi mkubwa wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) kutokana na faida zake kiuchumi ila kwa sasa kuna maeneo ambayo Serikali inayafanyia kazi kwa kina kupitia majadiliano na Wawekezaji ili mradi husika uwe na tija kwa nchi na wananchi.

Ameyasema hayo tarehe 29 Aprili 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Wabunge kuhusu Hotuba ya Bajeti ya  Wizara ya Nishati ya shilingi Trilioni 2.2 kwa mwaka 2025/2026 kabla ya kupitishwa kwa kishindo na Bunge hilo kwa asilimia 100.

“ Mradi wa LNG umeanza kusemwa kwa muda mrefu na kila mmoja angetamani mradi huu ukamilike jana lakini lazima tukubaliane kuwa lazima tujadiliane kwa kina na wawekezaji ili kupata kilicho bora na kuleta tija, ninachotaka kuwahakikishia ni kuwa timu ya majadiliano ya Serikali na Wawekezaji wanaendelea na majadiliano na tunatarajia kuwa ndani ya mwaka huu 2025 kama tutakuwa tumemaliza masuala matatu yaliyosalia kujadiliwa, mkataba huo utasainiwa ili mradi uanze mara moja.” Amesema Dkt.Biteko

Ameongeza kuwa, Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan ana kiu ya kuona mradi huo  unaanza na alishatoa maagizo kwa Wizara ya kuhakikisha kuwa mradi unaanza kutekelezwa.

Akijibu hoja kuhusu vituo vya mafuta vinavyoongezeka na kujengwa kwa kukaribiana,

Dkt.Biteko amesema kuwa Wizara ya Nishati imeanza mazungumzo na Wizara ya Ardhi ili kuongeza umbali kati ya kituo kimoja na kingine kutoka mita 200 za sasa kwa lengo la kuleta usalama wa watu, mazingira na shughuli za kijamii.

Kuhusu msamaha wa kodi mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa gesi inayotumika kwenye vyombo vya moto kama vile magari (CNG), Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali ilishatoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa vifaa na mashine mbalimbali zinazotumika katika mnyororo wa thamani kwa miradi ya CNG kama vile mitungi ya CNG pamoja na vifaa vya kuwezesha kufunga mfumo kuwezesha magari kutumia gesi hiyo.

Ameongeza kuwa, katika mwaka 2024/2025 Wizara ya Nishati imewasilisha Wizara ya Fedha mapendekezo ya maboresho ya kodi katika gesi asilia inayotumika kwenye magari ili kuzidi kuhamasisha matumizi ya CNG na wawekezaji wanaowekeza kwenye miradi hiyo wapate faida na kurudisha gharama wanazowekeza kwa haraka.

Akijibu  hoja za Wabunge kuhusu gharama za kuunganisha umeme vijijini na mijini, Dkt.Biteko amesema kuwa imeundwa timu kwa ajili ya kuangalia namna gani gharama hizo zitapunguzwa lengo likiwa ni kuleta unafuu kwa wananchi.

Kuhusu usambazaji wa umeme Vijijini, Dkt.Biteko amesema kuwa, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anapaswa kupongezwa kwa kufikisha umeme katika Vijiji vyote 12,318 kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 huku kazi ya kupeleka umeme vitongojini ikiendelea kwa kasi.

Akizungumzia ujenzi wa vituo vya kupoza umeme katika wilaya zote nchini kupitia mradi wa gridi imara, Dkt. Biteko amesema kuwa tayari Serikali imeshanunua viwanja kwa ajili kujenga vituo hivyo na katika awamu ya kwanza vitajengwa vituo 14 huku utekelezaji ukiendelea na katika laini za umeme ambazo ni ndefu sana Serikali itaweka switching stations.

Aidha, kuhusu suala la kukatika kwa umeme nchini, Dkt.Biteko amesema kuwa  limepungua kwa asilimia 48 huku dakika za kukatika umeme zikipungua kwa asilimia 64 na kwa sasa umeme ukikatika ni kwa sababu tu ya matengenezo ya miundombinu. Hata hivyo amesema Serikali inaendelea kuimarisha kituo cha huduma kwa  Wateja TANESCO ili taarifa ziwafikie wananchi kwa wakati pale umeme unapokatika ikiwemo kila wilaya kuwa na kundi sogozi.

Awali, wakati wa kuhitimisha Hotuba hiyo ya Wizara ya Nishati, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga alimpongeza Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya katika Taifa hususan kwenye Sekta ya Nishati akieleza kuwa moja ya misingi ya ukuaji wa kiuchumi na maendeleo katika Taifa lolote ni uwekezaji katika Sekta ya Nishati.

Akizungumzia mikoa ambayo bado haijaunganishwa katika gridi ya Taifa ya umeme, Kapinga alisema kuwa kuna miradi mbalimbali inayoendelea ambapo katika Mkoa wa Rukwa kuna mradi mkubwa wa kusafirisha umeme unaoendelea wa kutoka Iringa-Tunduma hadi Rukwa na kipande kingine cha mradi kitakachounganisha gridi ya Tanzania na Zambia.

“Mhe.Spika  katika Mkoa wa Mtwara na Lindi tayari mkandarasi yupo eneo la kazi, mradi umeanza kwa kujenga njia ya umeme kutokea Songea-Tunduru-Masasi hadi Mahumbika na tumeshaanza kulipa fidia katika eneo la Tunduru hadi Masasi takriban shilingi bilioni 4.6 na eneo lililobakia la Songea kuelekea Namtumbo na Tunduru tutaendelea kulipa fidia ya takriban shilingi bilioni 2.7.” Alisema Kapinga

Kuhusu kupeleka gridi ya Taifa katika Mkoa wa Kagera alisema kuwa kazi inaendelea kupitia ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya Benaco-Kyaka na katika Mkoa wa Katavi mradi wa kupeleka umeme wa gridi mkoani humo uko katika hatua za mwisho.

Akizungumzia kazi ya kupeleka umeme kwenye visiwa mbalimbali nchini, Kapinga alisema kuwa, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 9.89 ili kupeleka mifumo ya umeme jua katika visiwa 118 ambavyo vipo katika mikoa zaidi ya mitano hususan Wilaya ya Ukerewe.

Kuhusu maboresho miundombinu ya umeme katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Kapinga alieleza kuwa kuna kazi zinaendelea kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata umeme wa uhakika ikiwemo uboreshaji wa kituo cha Mbagala ambacho kilikuwa na transfoma yenye uwezo wa MVA 50 lakini sasa inawekwa transfoma mpya yenye uwezo wa MVA 120 ili kukiongezea uwezo kituo hicho ili wananchi wa Mbagala, Temeke, Yombo, Mkuranga na baadhi ya maeneo ya Kigamboni waendelee kupata umeme wa uhakika.

Alieleza kuwa kazi hiyo imefikia mwishoni na muda wowote transfoma hiyo itaanza kufanya kazi. Kwa eneo la Kigamboni amesema maboresho pia yanaendelea kufanyika na kwamba wananchi tayari wameshaanza kuona mabadiliko ya upatikanaji umeme kupitia maboresho hayo.

Comments

#maratotv

RAIS RUTTO AAMBATANA NA ODINGA NCHINI CHINA

Rais wa Jamhuri ya Kenya Mh William Rutto na mke wake wamewasili nchini China kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali wa Jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC). Katika ziara hiyo ameambatana na waziri mkuu mstaafu wa nchi hiyo Raila Odinga ambaye pia anapigiwa kampeni ili aweze kushinda nafasi ya Uenyekiti wa AU.

WIZARA YA MALI ASILI YASISITIZA MATUMIZI YA SHERIA NA KANUNI KATIKA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA UHIFADHI

Na.Joyce Ndunguru, Morogoro. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba asisitiza matumizi ya sheria na kanuni katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za uhifadhi. Kamishna Wakulyamba ameyasema hayo leo Septemba 1, 2024 wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya katika ofisi za Makao Makuu ya TAWA yaliyopo Mkoani Morogoro kwa lengo la kuongea na watumishi ili kuimarisha utendaji kazi pamoja na kukagua maeneo ya kazi. "Kama wahifadhi tunapaswa kufahamu sheria zote zinazosimamia masuala ya uhifadhi zilizopo katika Taasisi zetu pamoja na za Taasisi zingine za uhifadhi zilizopo ndani ya Wizara ya Maliasili na utalii" amesema Kamishna Wakulyamba. "Pamoja na kufahamu sheria na kanuni zilizopo ndani ya Wizara yetu, ni vyema kufahamu na kuzingatia sheria nyingine za Nchi ambazo zinatuzunguka ili ziweze kutusaidia katika utekelezaji wa majukumu yetu mfano sheria inayohusiana na ukusanyaji wa vielelezo kuanzia kw...

Rais Dkt. Samia Awasili China Kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano Kati ya China na Africa FOCAC

  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Beijing Capital nchini China kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) tarehe 03 Septemba, 2024.

Wananchi Serengeti Wamtaja Dkt Rhimo Nyansaho Kama Chachu ya Maendeleo Kwao

Na Shomari Binda-GMTV  WANANCHI Wilaya ya Serengeti mkoani Mara wamemtaja Dkt.Rhimo Nyansaho kama chachu ya maendeleo kupitia taasisi yake ya Nyansaho Foundation. Wakizungumza kwa nyakati tofauti na GMTV wananchi hao wamesema kwa kipindi kirefu mchango wake umeonekana katika kuisaidia jamii. Wamesema ukifika Jimbo la Serengeti kila Kata na Kijiji huwezi kukosa mkono wa Dkt.Nyansaho kuchangia na kusaidia jamii kuanzia elimu,afya,maji na masuala mengine ya jamii. Mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Mwita Sagati amesema wapo watu wanaojitokeza kusaidia jamii kipindi cha uchaguzi kwa kulenga kupata uongozi lakini imekuwa tofauti kwa Dkt.Nyansaho. Sagati amesema iwapo atajitokeza kuomba nafasi ya ubunge wapo tayari kumpambania na kumchagua ili aweze kuendelea kutoa mchango wake katika kusaidia jamii. " Tunashukuru sana mchango wa Dkt.Nyansaho kwa kuchangia shughuli za maendeleo hapa Serengeti. " Wengine huwa wanakuja nyakati za uchaguzi lakini huyu mchango wake ni ...

Meli ya Mv. Serengeti yapinduka na kuzama katika Bandari ya Mwanza kusini

 Meli Mv.Serengeti imepinduka na kuzama kwenye bandari ya mwanza kusini.  Meli hiyo imepinduka na kuzama disemba 26 majira ya saa Saba za usiku.  Tukio hilo limetokea meli hiyo ikiwa imefungwa katika gati la bandari ya mwanza kusini.  Kampuni ya meli Tanzania(Tashico) imethibitisha meli ya Mv. Serengeti kupinduka na kuzama upande mmoja wa nyuma.  Kwa Mujibu wa Taarifa iliyotolewa na kitengo cha Masoko na Uhusiano kwa Umma cha Kampuni hiyo inaeleza kuwa Tashico imeshirikiana na Timu mbalimbali za Wataalam kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania(TASAC), Mamlaka ya Usimamizi wa bandari (TPA) na wadau wengine katika Juhudi za Uokoaji.  Kwa Mujibu wa Taarifa hiyo,Taarifa rasmi ya chanzo cha Tatizo itatolewa Meli hiyo itakapokuwa imeinuliwa na Uchunguzi wa kubaini Tatizo utakapokuwa umefanyika. Meli ya Mv.Serengeti inadaiwa kusitisha safari zake kwenye ziwa Victoria mwaka 2016  Meli ya Mv.Serengeti imepinduka na kuzama katika...

MAKOMANDOO MIAKA 60 YA JWTZ,HAIJAWAHI KUTOKEA

Makomandoo ya jeshi la ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ)wamekuwa kivutio cha aina yake kwenye kikele cha maadhimisho ya miaka 60 ya tangu kuanzishwa kwa jeshi hilo. Katika sherehe hizo ambazo zimefanyika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshiriki kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika uwanja huo wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 1 Septemba, 2024. Rais ameonesha kujivunia na kulipongeza JWTZ kwa kufanya kazi kwa kufuata misingi ya kuanzishwa kwake huku akitumia nafasi hiyo kuwapongeza Marais waliomtangulia kwa kazi kubwa waliyofanya wakati wa uongozi wao kwa kuliongoza vema jeshi hilo.

Mbunge wa Bukoba Vijijini ameaga Sifa Kedekede Kwa Rais Samia

 Na Angela Sebastian; Bukoba  MBUNGE wa jimbo la Bukoba vijijini Dk. Jasson Rweikiza amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya wananchi wa jimbo hilo, kwa kuwapatia zaidi ya shilingi bilioni 19 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja mawili ambayo ni lango la kutoka na kuingia ndani ya mkoa wa Kagera. Ametoa shukrani hizo wakati akiongea wananchi mbalimbali waliofika katika viwanja vya Rweikiza pre and Primary school iliyoko eneo la Kyetema Bukoba vijijini, kwa kwa ajili ya kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa baba wa mbunge huyo aliyekuwa akiitwa Samsoni Rweikiza.  Rweikiza amebainisha kuwa,Dk. Samia Suluhu Hassan ni Rais mwenye upendo amekubali kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya Bukoba Vijijini na ndiyo maana tunasema atakuwa kiongozi wetu kwa awamu nyingine tena,tunapaswa kila mmoja kumuunga mkono. ametaja madaraja hayo kuwa ni Karebe ambalo limetengewa kiasi cha shilingi bil.9.3 kwa ajili ya ukarabati mkubwa kutokana na daraja ...

Jenerali Jacob Mkunda Atembelea Meli Tiba ya China Aridhishwa na Huduma

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda ametembelea meli tiba ya Jeshi la Ukombozi la Watu wa China Peace Ark ili kuona matibabu yanavyofanyika. Jenerali Mkunda amefurahishwa na namna wataalam wa tiba wa Jeshi la China walivyotoa matibabu kwa kushirikiana na wataalam wa tiba wa JWTZ . Meli tiba ya jeshi la China imekuja hapa nchini na kutia nanga kwenye bandari ya Dar Es Salaam kutoa matibabu mbalimbali kwa wananchi ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa JWTZ  na ushirikiano wa miaka 60 baina ya JWTZ na Jeshi la Ukombozi la Watu wa  China. Matibabu hayo yalianza kutolewa tarehe 18 Julai 2024 hadi tarehe 22 Julai 2024. Meli tiba hiyo itaondoka hapa nchini tarehe 23 Julai mwaka huu.

AMIRI JESHI MKUU AKAGUA GWARIDE LA MIAKA 60 YA JWTZ

 Mapema leo asubuhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Mhe.Dkt,Samia Suluhu Hassan akikagua Gwaride Maalumu la Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Uwanja wa Uhuru leo September 01,2024. Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa jeshi la ulinzi la Wananchi Tanzania si jeshi la Uvamizi bali ni jeshi la ulinzi wa Wananchi Tanzania Amewahakikishia wanajeshi kufanya kazi kifua mbele,kuwa amiri jeshi mkuu yuko pamoja nao wakati wote.

Jenerali ameacha alama ya uzalendo na kujitoa kwa ajili ya Taifa

*📌 Serikali itaenzi na kuthamini mchango wake* *📌 Asema Jenerali Musuguri alijitolea kuhakikisha Tanzania inabaki na amani na usalama* *📌 Asema alikuwa mstari wa mbele kuliokoa Taifa* *📌 Aiasa jamii kuacha alama katika maisha ya kila siku* *📌 Dkt. Biteko aongoza mamia ya watu mazishi ya Jenerali Musuguri Butiama* Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa  aliyewahi kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Mstaafu David Bugozi Musuguri alijitolea  kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa na amani, usalama na mshikamano pamoja na kuifundisha jamii  moyo wa dhati wa kuilinda nchi. Dkt. Biteko amesema hayo leo Novemba 4, 2024 Butiama mkoani Mara wakati akiwasilisha salamu za Serikali kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Jenerali Mstaafu Musuguri. “ Katika  uhai wa kila mmoja wetu ni jambo gani mtu atakumbukwa nalo, baba huyu a...