Na Ada Ouko ;Musoma.
MAMLAKA ya mapato mkoa wa Mara imefanikiwa kukusanya shilingi 142.98 bilioni kati ya shilingi 113.51 bilioni iliyolenga kupata kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/ 2024.
Sababu za kufikia lengo hilo zimetajwa kuwa ni mazingira mazuri ya biashara yaliyowekwa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi thabiti wa Raisi Dk Samia Suluhu Hassan na ushirikiano mzuri kutoka kwa wafanyabiashara, sambamba na uboreshaji wa mifumo ya tehama ambao umerahisisha ukusanyaji wa mapato hayo ya serikali.
"Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 tulikuwa na lengo la kukusanya kiasi cha shilingi 113.51 bilioni na tulifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi 142.98 bilioni ambayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 126 ya lengo"
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Mamlaka hiyo mkoani hapa Nasoro Ndemo leo february 7 mwaka huu 2025 kwenye maadhimisho ya siku ya walipa kodi yaliyofanyika katika ukumbi wa MK kata ya Mwisenge Manispaa ya Musoma.
Aidha, pamoja na mafanikio hayo Nasoro amesema kuna changamoto ziliwakwamisha katika ukusanyaji huo wa mapato ya serikali ambapo ni wafanyabiashara kushindwa kuwasilisha ritani kwa wakati, kushindwa kulipa kodi zao kwa wakati huku wafanyabiashara wengine kukwepa kusajili biashara zao.
Amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024 / 2025 mkoa huo umepangiwa kukusanya kiasi cha shilingi 190.18 bilioni, na kwamba kwa kipindi cha nusu mwaka kutoka julai 2024 mpaka disemba 2024, mamlaka hiyo ilikuwa na lengo la kukusanya 94.63 bilioni na kwamba ilifanikiwa kukusanya shilingi 98.55 bilioni sawa na ufanisi wa asilimia 104.
Kwa upande wake Naibu Kamishna wa uwezeshaji biashara wa mamlaka hiyo nchini Wahabi Matengo amesema kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/ 2024 mamlaka hiyo imefanikiwa kukusanya shilingi Trilioni 27.64 sawa na asilimia 97.67 ya lengo la kukusanya shilingi Trilioni 28.39 , makusanyo ambayo ni ongezeko la asilimia 14.5 ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi trilioni 24.4 kilichofikiwa katika mwaka wa fedha 2022/2023.
Maadhimisho ya shukrani kwa mlipa kodi hufanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa shughuli na matukio mbalinbali, kama vile matembezi ya hisani na walipa kodi, watumishi wa mamlaka ya mapato, wakuu wa taasisi na idara mbalimbali za serikali, wawakilishi wa vyama na makundi mbalimbali ya wafanyabiashara nchini.