Na Angela Sebastian ;Bukoba
MAMLAKA ya mapato Tanzania( TRA) mkoani Kagera imeadhimisha wiki ya shukrani kwa mlipa kodi kwa kutoa misaada ya vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni tano kwa watoto yatima na wasiojiweza katika kituo cha watoto Yatima cha Uyacho kilichopo Manispaa ya Bukoba mkoani humo.
Meneja wa TRA mkoani Kagera Castor John amesema wametoa vitu hivyo kwa watoto hao vyenye thamani ya shilingi ikiwa ni kurudisha shukrani kwa mlipa kodi wakiamini kuwa watoto hao ni wadau pia wanamchango mkubwa katika ulipaji wa kodi kupitia huduma wanazopatiwa ikiwemo za manunuzi ya vitu mbalimbali.
Maadhimisho hayo kwa kufanya matembezi yaliyoanzia katika ofisi za TRA mkoa huo na kupita mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Bukoba kwa kujumuisha wadau wa mamlaka hiyo waliobeba mabango yenye ujumbe wa kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari na shukrani kwa mlipa kodi.
Misaada iliyotolewa ni pamoja na mchele, sukari, unga, maharage, mafuta ya kula, unga wa ngano, sabuni za unga, sabuni za miche, mafuta ya kupaka, juice, soda, pipi, daftari, daftari, kalamu, penceli, kalamu, chunvi na maziwa ya unga.
John amesema kuwa katika wiki ya shukrani kwa mlipa kodi mbali na mambo mengine yote ya kikodi wanayofanya ni kurudisha shukrani kwa mlipa kodi ambapo watoto hao ni wadau pia.
"Kwanini tunarudisha kwa jamii kwanza kuwatia moyo ninyi ambao mmechukua jukumu la kuwatunza watoto hawa kwa sababu siyo kila mtu anaweza akafanya, unafanya kitu ambacho wakati mwingine unafanya kwa matumaini mnapaswa kutiwa moyo hii ni ibada pia ni matendo ya huruma" amesema John
Anasema watoto ni sehemu ya jamii pia watoto hawa ni walipa kodi wetu wakienda kununua vitu dukani kwa mtu ambaye anachangia vat analipa kodi pamoja na kwamba wako hapa lakini ni walipa kodi wetu mnatusaidia kuwalea.
Naye mratibu wa kituo cha Uyacho Sadath Kachwamba amesema kuwa, kituo hicho kimeishalea watoto zaidi ya 412 tangu kilipoanzishwa mwaka 1998 hadi sasa na waliopo kwa sasa ni watoto 72 na wengine wapo shule,vyuo na makazini.
Ameongeza kwamba, wana watoto zaidi ya saba wameishaajiliwa serikalini, watoto zaidi ya 30 wameishajiajili, watoto wanne wako hospitali ya Muhimbili wanachukua kozi mbalimbali za udaktari, vyuo vikuu vya Dodoma na Dar es salaam.
Halima Jamali ni mtoto anayelelewa katika kituo hicho ametoa shukrani kwa msaada uliotolewa kituoni hapo na kuwaombea kwa Mungu ili aendelee kuwawesesha hata siku nyingine warudi na kutoa misaada kituoni hapo.
Pia Halma amewaomba wadau na taasisi za serikali na zisizo za serikali kwenda kuwatia moyo na kuwashika mkono ili kutatua changamoto walizonazo katika kituo hicho ambazo ni vitanda 16, magodoro 32, blanketi 32, shuka 64 na mito 32.













Comments
Post a Comment