Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Visiwa vya Comoro Mheshimiwa Saidi Yakubu,februari 11 Mwaka huu amekutana na kufanya Mazungumzo na Ujumbe maalumu kutoka Serikali ya Comoro unaoshughulikia azma ya nchi hiyo kuimarisha biashara ya bidhaa za chakula.
Ujumbe huo uliongozwa na Bw. Snehal SONEJI, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa nchini Comoro.
Washiriki wengine kwenye Mazungumzo hayo ni Dkt. Hamza A. Azali, Mamlaka ya Utafiti wa Kilimo, Mazingira na Uvuvi (INRAPE), na Bw. Abdillahi M'Saidie, Rais wa Jumuiya ya Wafugaji, Wakulima, Wavuvi na Sanaa nchini Comoro.
Ujumbe kutoka Serikali ya Comoro ulijulisha kuwa ulitembelea Tanzania wiki ya kwanza ya mwezi Februari, 2025 ambapo walibahatika kukutana na kufanya mazungumzo na watendaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kukutana na Ushirika wa Uzalishaji katika Chuo cha Kilimo cha SOKOINE, pamoja na kutembelea miradi ya kilimo.
Kufuatia mazungumzo yao, Taasisi za Tanzania zimeonesha utayari wa kushirikiana na Comoro,hivyo Mamlaka za Comoro zinakamilisha taratibu za ndani kuwezesha bidhaa kuingia nchini Comoro na baadae kuweka utaratibu utakaowezesha uzalishaji wa bidhaa nchini mwao.
Aidha, Ujumbe huo umejulisha kuwa ulipata fursa ya kukagua mfumo wa usafirishaji wa bidhaa kati ya Tanzania na Comoro na kubaini baadhi ya changamoto ya upakiaji wa mizigo na ukosekanaji wa huduma ya bima ya mizigo ambapo wameomba Mamlaka za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutafutia ufumbuzi changamoto zilizopo.
Naye Mheshimiwa Balozi Saidi Yakubu amepongeza juhudi zinazochukuliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini Comoro katika kusaidia utekelezaji wa mipango ya maendeleo nchini humo.
Balozi Yakubu ameahidi kuwa Ofisi yake itaipatia ushirikiano UNDP ili kuwezesha kufikia malengo ya Taasisi hiyo.
Aidha, amefahamisha kuwa Ofisi yake imepokea taarifa na tathmini kamili ya ujumbe huo na kusisitiza kwamba ataelekeza waasaidizi wake kuangalia namna ya kuwasiliana na Mamlaka za Tanzania ziweze kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na kukamilisha maazimio yaliyofikiwa katika mazungumzo yaliyofanyika wakati wa ziara hiyo.
Mheshimiwa Balozi Saidi Yakubu ameuhakikishia Ujumbe kutoka Comoro kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itashirikiana na mamlaka wenyeji kuhakikisha usalama wa chakula nchini Comoro, kuimarisha uzalishaji wa ndani na kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili sekta ya biashara na usafirishaji kati ya nchi mbili hizi.










Comments
Post a Comment