Juhudi Za Kuboresha Ikolojia Hifadhi Ya Taifa Ziwa Manyara Zazaa Matunda, Wanyama Wazidi Kuongezeka

GEORGE MARATO TV
0


 Na. Happiness Sam - Manyara

Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wamepongeza juhudi za Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara katika kuboresha ikolojia ya maeneo yake, hatua iliyochangia ongezeko la wanyama katika Hifadhi hiyo.

CPA. Khadija Ramadhani ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi alitoa pongezi hizo leo februari 06, 2025 wakati wa ukaguzi wa maeneo hayo, ukaguzi uliyofanyika ndani ya hifadhi hiyo iliyopo mkoani Manyara.

Akiwa katika ziara hiyo CPA. Khadija alisema, “Niwapongeze Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara kwa juhudi kubwa za kuboresha mazingira na ikolojia ya maeneo mbalimbali katika Hifadhi hii, hali iliyopelekea ongezeko la wanyama tofauti na hali ilivyokuwa hapo awali”.

Aidha aliongeza, “Leo tumeshuhudia Twiga, Pundamilia, Tembo na Swala wengi, niwapongeze kwa kazi nzuri ya kuendelea kuyalinda maeneo ya Hifadhi zetu na kuboresha maeneo yenye misitu minene kwa kuyawekea “fireline” ili moto unapowaka katika Hifadhi hii ukifika kwenye maeneo haya uweze kuzima kwa urahisi ili kupunguza madhara makubwa katika rasilimali hizi na pia kuondoa mimea vamizi hali ambayo imeimarisha malisho ya wanyama”.

Akizungumza wakati wa kupokea Wajumbe hao wa Bodi ya Wadhamini -TANAPA, Naibu Kamishna wa Uhifadhi Steria Ndaga ambaye ni Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini alisema kuwa jitihada hizi zimeendana sanjari na uboreshwaji wa miundombinu ili kurahisisha shughuli za utalii na ulinzi wa maliasili.

Vilevile, Kamishna Ndaga aliongeza “ Sasa hivi barabara nyingi za Hifadhi ya Manyara zinapitika mwaka mzima pawepo jua ama mvua na hii imechochea ongezeko la watalii kutembelea maeneo yenye vivutio mbalimbali, na kusababisha watalii wengi wanaotembelea Hifadhi ya Manyara kutoa maoni ya kuwa ni Hifadhi nzuri na watakapopata nafasi watarudi tena.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Yustina Kiwango ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara alisema, “ Sisi kama Hifadhi tunaahidi kufanya kazi kwa bidii na kutekeleza majukumu yetu kwa wakati na kwa ufanisi wa hali ya juu kuleta tija kwa shirika letu na kwa Taifa kwa ujumla.

Aidha, Kamishna Kiwango aliongeza kuwa kama hifadhi wataendelea kutatua changamoto zinazoikumba Hifadhi hiyo, kusimamia ulinzi wa maliasili, kutoa huduma bora kwa wageni pamoja na kutunza mazingira ili ikolojia ya Hifadhi hiyo iendelee kuwa rafiki kwa wanyama kuzaliana na kuongezeka kwa ajili ya manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top