CV ya Dkt. Nchimbi imeshiba Mno, anatosha Kwenda Kuwa Msaidizi wa Kwanza wa Rais Samia

GEORGE MARATO TV
0




Na Bwanku M Bwanku.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoongoza Taifa Tanzania kimekua na wiki ya aina yake kuanzia Jumamosi na Jumapili Januari 18 na 19, 2025 kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.

CCM imekua na Mkutano Mkuu wake Maalum ambao ulikua na ajenda mbalimbali kubwa ikiwa kumchagua Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho baada ya aliyekua akishika nafasi hiyo Ndugu Abdulrahman Kinana kujiuzulu, hatimaye Ndugu Stephen Masatu Wasira akachaguliwa kuziba nafasi hiyo.

Kwenye Mkutano Mkuu huu Maalum licha ya ajenda zake Mama zilizokua zinajulikana na shughuli zilizofanyika kama hiyo ya kumchagua Makamu Mwenyekiti, kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Chama na mabadiliko madogo kwenye Katiba yake, kumpitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mgombea Urais wa CCM na Dkt. Hussein Mwinyi kuwa Mgombea Urais wa CCM Zanzibar, Mkutano huu umefanya jambo lingine kubwa ambalo halikutarajiwa na yeyote na kutikisa Taifa wakati huu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu hapo baadae.

Kwa mshangao mkubwa, bila kujulikana wala kutarajiwa na yeyote, hatimae Mkutano Mkuu huu umemthibitisha Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi kuwa Mgombea Mwenza wa CCM wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2025.


Hili linatokea baada ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango na ambaye alitarajiwa kuwa Mgombea Mwenza wa Dkt. Samia kwenye Uchaguzi Mkuu kuomba na kuandika barua kwa Rais Samia ya kupumzika na hatimaye ndani ya Mkutano huo kikafanyika kikao cha haraka haraka cha Kamati Kuu ya CCM ambacho kilikuja na jina la Dkt. Nchimbi na Mkutano Mkuu kumthibitisha papo hapo. Hakuna aliyetarajia, Taifa limepata mshangao mkubwa sana. 

Imekua ghafla na historia bila ya kutarajiwa na yeyote CCM kwenye Mkutano Mkuu wake huu ambao hata haukua na ajenda hiyo kumpata Mgombea Mwenza atakayesimama na Rais Samia kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka huu 2025 ambaye ni Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi.


Sasa, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ni nani?

Jina la Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi sio jina geni kwenye anga la siasa za Tanzania. Ni moja ya wanasiasa wakubwa, mahiri na wakongwe wanaoendelea kuteka uga huu wa siasa za Tanzania. 

Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi ni moja ya wanasiasa wakubwa sana kwenye siasa za Tanzania. Kwa utumishi na uzoefu wake mkubwa ndani ya CCM na serikali akiwa na zaidi ya miaka 35 akishika nafasi kubwa na nyeti za maamuzi.

Ndiye Katibu Mkuu wa CCM kwasasa, Chama kinachoongoza Taifa hili.
 
Ameshika nafasi mbalimbali kwenye ngazi za chini na za msingi za CCM, akiwa Chuo mwaka 1997 alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mwaka mmoja mbele 1998, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Jumuiya aliyoiongoza mpaka mwaka 2008. Pia amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda iliyoko mkoani Mara wakati wakati wa Awamu ya 3 ya Hayati Benjamin Mkapa kuanzia mwaka 2003 hadi 2005.

Kuwa Kiongozi Mkuu wa Jumuiya hiyo ya Vijana kwa ngazi ya Taifa, moja kwa moja kukampa tiketi ya kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Halmashauri Kuu (CC & NEC). Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM ni moja ya vikao vya juu kabisa vitatu vya CCM kando ya Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ambavyo vinafanya maamuzi makubwa ndani ya Chama hicho ikiwemo kumpitisha Mgombea Urais wa CCM, Mwenza, Wabunge lakini vikiwa ni vikao vinavyojadili hali ya CCM na utekelezaji wa Ilani yake na serikali na mengine mengi makubwa yanayogusa maslahi ya Taifa zima. 

Baada ya kuhudumu kwenye nafasi kubwa ndani ya Chama na zenye maamuzi makubwa ndani ya Chama na Taifa, Mwaka 2005 Dkt. Nchimbi aligombea Ubunge kwenye Jimbo la Songea Mjini na kushinda ambapo moja kwa moja Rais wa Awamu ya 4 wa kipindi hicho Dkt. Jakaya Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri kwenye Wizara 3 akianza kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo kuanzia Januari 2006, kisha Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana mwaka huohuo Oktoba pamoja na Naibu Waziri wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa alikohudumu kuanzia Februari 2008 hadi 2010 kwenye Uchaguzi Mkuu. 

Mwaka 2010 aligombea tena na kushinda na hapo sasa Rais wa Awamu ya 4 Dkt. Jakaya Kikwete akamteua kuwa Waziri kamili akianza kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo na baadae Waziri wa Mambo ya Ndani.

Mwaka 2016, Dkt. Nchimbi aliteuliwa na Aliyekuwa Rais wa Awamu ya 5 Hayati John Magufuli kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil kabla ya baadae mwaka 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kumbadilishia Kituo cha kazi ya Ubalozi kwa kumteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri, nafasi aliyohudumu mpaka mwaka Jana 2023 alipomaliza muda wake na kurudi nchini kwa mujibu wa sheria.

Baada ya kazi kubwa akianzia ngazi za chini za uongozi, Uenyekiti wa Jumuiya ya Vijana Taifa (UVCCM), Mbunge, Naibu Waziri hadi Waziri kamili na Ubalozi hatimaye Januari 15, 2024 Dkt. Nchimbi aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Mtendaji Mkuu wa Chama hiki kinachoongoza Taifa letu Tanzania

Anasifika kwa misimamo madhubuti isiyoyumba (hili nitalichambua) akiwa na ushawishi mkubwa ndani ya Chama na Nje hasa kwa kufanya kazi ndani na Nje ya Nchi. 

Kwa CV yake hii ilivyoshiba akishika nafasi kubwa na nyeti akianzia ngazi za chini, ni mtu madhubuti kuweza kuwa msaidizi namba moja wa Mkuu wa Nchi.

Ni ukweli usiopingika kwamba kwa Rais kariba ya Dkt. Samia anayefanya mageuzi makubwa ya maendeleo ndani ya nchi anahitaji kuwa na wabobezi wakubwa wa siasa na utumishi kumsaidia kutafsiri maono yake.


Balozi Nchimbi ni Msomi mzuri aliyebobea kwenye masuala ya Fedha na Benki akihitimu Shahada ya Uzamivu (PHD) kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2011.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top