Vitendo Vya Ukatili wa Kijinsia Mkoa wa Mara Ukiwemo na Ukeketaji Vimeshuka Hadi Kufikia Asilimia 28
Fresha Kinasa- Mara
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema mkoa wa Mara umeendelea kupiga hatua katika kupambana na vitendo vya Ukatili wa Kijinsia ukiwemo ukeketaji ambao umeshuka hadi asilimia 28, na kutoka nafasi ya kwanza kama ulivyokuwa hapo awali. Huku mikoa ya Arusha na Manyara ikiitaja kuongoza hapa nchini kwa kufungana kwa kuwa na asilimia 43.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo Dicemba 9, 2024, katika kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa Kijinsia Kitaifa zilizofanyika Uwanja wa shule ya Sekondari Ingwe Nyamongo Wilayani Tarime Mkoani Mara. Huku akisema ukeketaji umepungua kwa kiwango Cha asilimia 2 kitaifa.
Ambapo wadau mbalimbali kutoka Serikalini, Mashirika ya Kiraia, Taasisi za Dini, Wazee wa Kimila, na Wananchi wameshiriki katika kilele hicho chini ya kauli mbiu ya mwaka huu isemayo "kuelekea miaka 30 ya Beijing chagua kutokomeza ukatili wa Kijinsia''
Dkt. Gwajima amesema, Mkoa wa Mara kwa sasa umeendelea kupiga hatua tofauti na awali ambapo vitendo hivyo vilikuwa vimeshika kasi. Huku akihimiza Wananchi kuendelea kuachana na mila na desturi zinazochochea vitendo hivyo ambavyo vinarudisha nyuma juhudi za maendeleo.
"Ukeketaji Mara umeendelea kupungua kwa mujibu wa Tafiti za kitaifa za Idadi ya Watu na Afya Tanzania za mwaka 2022, Mkoa wa Mara una asilimia 28, maeneo mengine umeshuka asilimia kwa asilimia 2 na maeneo mengine umepanda, wakati Mkoa wa Arusha una asilimia 43, Manyara asilimia 43, Singida asilimia 20, Tanga asilimia 19, na Dodoma asilimia 18. Napongeza Mkoa Mara kuendelea kufanya juhudi kupunguza kiwango Cha ukeketaji."amesema Dkt. Gwajima.
"Mambo ya ukatili, Tuanze kuiondoa Mara kwenye sura ya ukatili wameshaitikia, elewa pasi na shaka kwa sababu ya Viongozi wenu wakuu wote wanashirikiana pamoja na Jamii na Wazee wetu wa kimila."amesema Dokt. Gwajima.
Aidha, ameyataka Mashirika ya Kiraia na Wadau wa mapambano ya Ukatili wa Kijinsia kuongeza Kasi ya utoaji wa elimu hasa kwa wanawake wanaoishi Vijijini kwani ndiko idadi kubwa ya vitendo vya Ukatili vimekuwa vikifanywa na Serikali itazidi kushirikiana na taasisi zote na Jamii nzima kujenga Taifa imara lisilo vitendo vya ukatili.
Aidha amewashukuru Wazee wa Kimila kutoka Koo 12 za kabila la kikurya kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali kupiga vita vitendo vya ukeketaji na amewahimiza kuzidi kutoa elimu katika Jamii akisema madhara ya ukatili yanarudisha nyuma juhudi na jitihada za maendeleo na kuhatarisha afya na usalama wa wanawake hasa wanaokumbana na ukeketaji, vipigo ndoa za utotoni na ukatili mwingine.
Kwa upande wake Mark Njera Ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara amesema kuwa "Msimu huu ni wa ukeketaji, Koo tisa Kati ya Koo 12 zinakeketa. Kwa kutambua jambo hilo kipindi hiki cha siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia elimu imetolewa na Maofisa wa Polisi Dawati la Jinsia na Watoto wapatao 150 kutoka Mikoa yote ya Tanzania ambapo walianza kitoa elimu hiyo kuanzia Dicemba 3, 2024, hadi Decemba 9, 2024."amesema na kuongeza kuwa.
"Elimu imetolewa kwa wanafunzi wa shule za Msingi wapatao 13,000, wanafunzi wa shule za Sekondari 11,000, kata 48, minada, makanisa na vikundi. Na katika kipindi hicho Wasichana 113, wameokolewa katika hatari ya kukeketwa, tunaomba serikali iweze kutunga sheria ya kushughulikia ukeketaji."amesema Kamanda Njera.
Naye Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijiji Mwita Waitara amesema ili kumaliza tatizo la ukeketaji ni vyema elimu inayotolewa iwe shirikishi kutokana na jambo hilo kuwa ni la kimila na pia mfumo dume bado upo. Huku akikiri ukatili kwa sasa umepungua kwani awali matukio mengi ya ukatili yalishamiri sana na wakati mwingine yalifanywa hadharani.
Apolinary Lyambiko ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barick North Mara amesema kuwa Mgodi huo umeendelea kushirikiana na Serikali na Wadau mbalimbali katika kupambana na ukatili wa Kijinsia ikiwemo kutoa elimu kwa Jamii na kuweka kipaumbele katika masuala ya Jinsia ili kuimarisha usawa wa Kijinsia katika Jamii.





Comments
Post a Comment