Misungwi yaadhimisha Miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika Kwa Kufanya Usafi wa Mazingira Kwenye Maeneo ya Umma
Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza imeadhimisha sherehe za miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya umma ikiwemo Kituo cha Magazine Misungwi,Solo kuu la Misungwi na Soko la Jioni la Gwambina.
Akizungumza na Wananchi na Watumishi walioshiriki kufanya usafi kati tarehe 9 Disemba 2024, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Johari Samizi amewataka wananchi kuendelea kufanya usafi katika maeneo yao sanjari na kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa na kuonya kuwa watakaopuuzia zoezi la usafi watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Mhe. Samizi ameongeza kuwa tangu kipindi cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere hadi hivi sasa yametendeka mengi ikiwemo Ujenzi wa Daraja la JPM, Shule za msingi na Sekondari, miradi ya maji, Vituo vya afya na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya iliyopo Iteja, pamoja na Barabara.
Kupitia awamu ya sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuna mabadiliko sana ambapo asilimia kubwa ya watu ni vijana ambao hawakushiriki harakati za uhuru mwaka 1961, ila wana wajibu wa kuitunza ili kuikabidhi kwa vizazi vijavyo Taifa likiwa salama katika shughuli za kimaendeleo na fursa mbalimbali zipatikanazo katika awamu ya sita.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Wilaya ya Misungwi Bw. Addo Missama pia ametumia fursa hiyo kuwasihii wananchi kuendelea kutoa ushirikiano katika juhudi za kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa safi ambapo kila mmoja anapaswa kujenga utamaduni wa kuhakikisha eneo lake linakuwa safi muda wote ili kupunguza athari za kupata magonjwa ya milipuko ikiwemo Kipindupindu.
Naye Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Misungwi Bi. Elly Makala mara baada ya kushiriki shughuli za usafi amesema kuwa katika kuadhimisha miaka 63 ya uhuru Tanzania bara,Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Nchini(TAKUKURU) itaendelea kuwashirikisha wananchi na kuwakumbusha kutoa ushirikiano katika kuzuia vitendo vya rushwa visitokee mapema ili kuwezesha kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo kwa ubora na viwango vinavyotakiwa kulingana na thamani ya fedha.
Naye Diwani wa Kata ya Misungwi Mhe. Mganyizi Feruzi amehimiza Ushiriki wa kila mwanajamii kwenye suala la usafi na kuwahimiza wananchi kutosubiri kuambiwa kuhusu usafi wa mazingira badala yake wafanye usafi kuwa sehemu yao ya maisha ili kuepuka magonjwa mbalimbali ya milipuko ikiwemo kipindupindu.
Mbali na usafi wa mazingira,Wilaya ya Misungwi imeadhimisha Sherehe za Uhuru mwaka 2024 kufanya Kongomano na mdahalo wa majadiliano ya Wananachi kuhusu maendeleo ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara lililofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ufundi na maendeleo ya jamii Misungwi.





Comments
Post a Comment