Waziri Gwajima alia na mbinu mpya za ukeketaji

GEORGE MARATO TV
0


Wakati serikali na wadau mbalimbali wakipiga vita vitendo vya ukeketaji,baadhi ya wakazi wa wilaya Tarime mkoani mwanza wanadaiwa kubuni mbinu mpya kwa ajili ya kukwepa mkono wa dola.

Miongoni mwa mbinu zilizobuniwa wilayani humo ni pamoja na kupunguza umri wa ukeketaji kufikia chini ya miaka mitano pamoja na kuwapeleka watoto kwenda kukeketwa nchi Jirani ya Kenya.

Mbinu hizo zimebainika katika kijiji cha borega kata ya Ganyange wakati wa kampeni ya kuamsha ari ya kutokomeza vitendo vya ukeketaji,mimba na ndoa katika umri mdogo pamoja na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Wakizungumza wakati wa kampeni hiyo,baadhi ya wakazi wa kijiji cha ganyange wameiomba serikali kuchukua hatua stahiki ili kukomesha vitendo vya ukeketaji.

Msimu wa ukeketaji unatarajia kufanyika wilayani Tarime mwishoni mwa mwaka huu ambapo Jeshi la polisi Mkoa maalum wa kipolisi Tarime rorya limesema kuwa tayari kwa kushirikiana na wadau mbalimbali  limetoa elimu ya kutosha kwa Jamii kuhusu madhara ya ukatili ukiwemo wa watoto.

Kamishna msaidizi wa polisi Joswan Kaijanate  amesema kuwa Jeshi hilo limejipanga kudhibiti vitendo vyote ambavyo ni kinyume cha sheria na kuwatahadharisha wazazi na walezi kutothubutu kukeketa watoto wao na watakaokaidi watakumbana na mkono wa dola.

‘’Tutumie fursa hii kuwaomba yale yote mliokuwa mnayafanya kwa kipindi cha nyuma kwa mwaka huu yasifanyike ili tusije kuanza kutafutana,hatutaruhusu na hatutakubali kuona vitendo vya kikatili dhidi ya watoto ikiwemo ndoa za umri mdogo,mimba za utotoni na ukeketaji vinaendelea Tarime’’alisema Kaijanane

Kampeni hiyo imeandaliwa na shirika la kutetea haki za wanawake na watoto la Kivulini ambalo limekiri kubadilika kwa mbinu za ukeketaji zimebadilika  ambapo asilimia 34 ya watoto wanakeketwa kabla kufikisha umri wa miaka mitano,asilimia 28 wanakeketwa wakiwa na umri wa miaka 10 hadi 14 huku wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wakikeketwa kwa asilimia nane.

Mkurugenzi mtendaji wa Kivulini Yassin Ally amesema kuwa Kwa mujibu wa Takwimu kutoka ofisi ya Taifa ya takwimu,asilimia 55 ya wanawake nchini hukeketwa na wakunga wa jadi tofauti na zamani ambapo wakeketaji walikuwa maghariba.

Yassin ameiomba serikali kuimarisha usimamizi wa wakunga wa Jadi ili baadhi yao wasiendelee kuwa chanzo cha ukatili dhidi ya watoto wa kike.

Kwa upande wake,Mkuu wa wilaya Tarime Meja Edward Gowele amesema kuwa ukeketaji na ubakaji ni miongoni mwa vitendo vya ukatili vilivyoshamiri wilayani humo kutokana na tatizo la mmomonyoko wa maadili.

Meja Gowele amesema kuwa moja ya hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kuimarisha ujirani mwema na nchi Jirani na Kenya ili kudhibiti watenda ukatili ikiwemo ukeketaji wanaokimbilia kenya


Akizungumza kwenye kampeni ya kuamsha ari ya kutokomeza vitendo vya ukeketaji,mimba na ndoa katika umri mdogo pamoja na ukatili dhidi ya wanawake na watoto,waziri wa maendeleo ya Jamii,Jinsia,wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima ameupongeza mkoa wa mara kwa kufanikiwa kupunguza vitendo vya ukatili.

Dkt.Gwajima amewataka wakazi wa mkoa mara kutembea kifua mbele na kuelezea mambo mema yaliyopo mkoani humo badala ya kuendeleza mambo yanayochafua taswira nzuri ya mkoa huo.


‘’Takwimu za ofisi ya taifa ya takwimu,mkoa mara umepunguza kwa mara ya kwanza ukatili wa kijinsia kutoka asilimia 78 hadi 66 mwaka 2016 hadi mwaka 2022,ukeketaji kutoka asilimia 32 hadi 28,mimba za utotoni kutoka asilimia 37 hadi 31 katika kipindi hicho’’alisema Waziri Gwajima na kuongeza kuwa

‘’matokeo ya kupungua kwa ukatili yanatokana na Juhudi na ushirikiano unaofanyika kati ya serikali na wadau wa maendeleo ikiwemo ndugu zetu wa kivulini,mi sijawahi kuona shirika liko active kwa kweli yaani nikiambiwa nichague matano kivulini yumo”

Waziri Gwajima amesema kuwa katika kudhibiti matukio ya ukatili dhidi ya watoto ikiwemo ukeketaji ni vyema sheria ya ulinzi wa mtoto ikafanyiwa mapitio ili kuimarisha usalama wa watoto ikiwemo kuchukua hatua stahiki dhidi ya watu wanaoendekeza vitendo hivyo.











 

  

 


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top