Wanafunzi Toka Bunda na Serengeti Wanufaika na Mafunzo ya Uhifadhi Maliasili na Mazingira Toka Grumeti Fund
Na Emmanuel Chibasa
Tafiti mbalimbali zilizofanywa na Taasisi ya Utafiti na Utetezi wa Haki za Ardhi (HAKIARDHI) pamoja na wadau wa mazingira na mashirika mengine kuanzia mwaka 2013 zinaonyesha viashiria vya kuthibitisha kuwepo kwa mabadiliko ya tabia nchi kutokana na Vipindi vya mvua kubadilika mara kwa mara, Kukauka kwa vyanzo vya maji, Ongezeko la joto pamoja na Kutotabirika kwa majira ya mwaka nk.
Mabadiliko ya tabia nchi ni mabadiliko ya hali ya hewa ya muda mrefu katika eneo fulani (Mkoa, Nchi au Bara) tofauti na iliyozoeleka na Mabadiliko hayo huleta athari katika nyanja za kiuchumi, kimazingira na kijamii, kutokana na mwenendo wa uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi yanatokana na uharibifu wa maliasili na mazingira.
Wataalamu wa masuala ya mazingira wameainisha vyanzo vya kiasili na shughuli za kibinadamu ambavyo vinasababisha mabadiliko ya tabianchi kutokea.
Miongoni mwa shughuli hizo za binadamu ni pamoja na uvunaji wa misitu usio endelevu kwa ajili ya biashara ya mbao na mkaa, Uvamizi wa misitu kwa ajili ya shughuli za kilimo, makazi, na ufugaji ambapo miti ya asili hukatwa, Uchomaji moto misitu na mbuga kwa ajili ya kurina asali, kuandaa mashamba na uwindaji wa wanyama wadogo ambayo hupoteza uoto wa asili na kutoa hewa ukaa.
Katika kupambana au kuhimili athari za mabadiriko ya tabia nchi katika wilaya ya Serengeti na Bunda mkoani Mara, Grumeti Fund walianzisha kituo cha elimu ya Mazingira cha Enviromental Education Centre(EEC) ili kutoa elimu ya uhifadhi wa Maliasili na Mazingira kwa wanafunzi wa shule za Sekondari ya wilaya hizo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa katika jarida la Sauti ya Grumeti toleo la 13 katika ripoti ya mwezi Julai-Septemba 2023, inaeleza kuwa kila mwaka wanafunzi 512 wa shule za sekondari wilaya ya Serengeti na Bunda, wanapatiwa elimu hiyo ambapo kila wiki wanafunzi wa kike na wakiume 16 wenye umri wa miaka 15 hadi 18 hufundishwa masuala mbalimbali yanayohusu uhifadhi na maliasili kwa vitendo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa tayari matunda ya elimu hiyo kwa wanafunzi imeanza kuonekana ambapo wanafunzi wa shule ya Sekondari Kunzugu wilayani Bunda, ambao pia walihudhuria mafunzo hayo wameanzisha mradi wa kitalu chenye miche 3,000 ya miti ambayo walipanda katika msimu wa mvua na miche mingine kuigawa katika shule nyingine ili kusaidia na kuunga mkono wa jitihada za kuhifadhi mazingira.
Pia faida nyingine wanayopata wanafunzi hao ni wakazi wa maeneo ya Kunzugu kununua miche hiyo kwa bei nafuu na pesa zinazopatikana zinatumika kuendesha kitalu hicho cha miti.
Wakati wanafunzi wa Kunzugu Sekondari wakiendelea na upandaji wa miti, wanafunzi wa shule ya Sekondari Rigicha wilayani Serengeti wao wana miradi ya ufugaji nyuki na utunzaji wa miti ya mpingo baada ya kupata elimu ya mazingira na kuona umuhimu wa uhifadhi wa miti hiyi hadimu na iliyo hatarini kutokweka.
Kupitia mradi huo wa ufugaji nyuki wanafunzi hao wanaweza kulina kati ya lita 40-60 za asali kwenye mizinga kumi na tano wliyonayo kila mwezi.
Mkuu wa kituo cha Mazingira(EEC) Laurian Lamatus, anasema matokeo ya elimu hiyo ya mazingira sio tu uchangia kutengeneza wahifadhi wa baadaye bali pia husaidia wanafunzi hao katika kuchagua mlengo wa kazi watakazofanya baadae.
“Mfano tuna wanafunzi waliopita kituoni hapa kwa Miaka kumi au kumi na tano iliyopita na sasa wanafanya kazi za uhifadhi kama vile mabwana misitu” Amesema Laurian
Katika hatua nyingine Laurian ameongeza kuwa kituo cha Elimu ya Mazingira EEC cha Grumeti Fund huweza kupokea wanafunzi 32 pekee kwa mwaka kutoka shule za Sekondari kumi na sita zilizoko kwenye mpangao huo na shule nyingi huwa na wanafunzi wengi hadi 700 na zaidi.
Ameongeza kuwa ili kuweza kuwafikia wanafunzi wengine, wanafunzi waliohudhuria mafunzo hayo huendesha midahalo ya mazingira mashuleni mwao, mashindano ya uchoraji na kuandika insha zinazohusu mazingira na uhifadhi.



Comments
Post a Comment