Waziri Mkuu Aweka Jiwe La Msingi Mradi Wa Kupoza Umeme Mkata – Tanga

GEORGE MARATO TV
0


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amekagua ujenzi wa mradi wa kupoza umeme uliopo Mkata, wilayani Handeni na kuweka jiwe la msingi la kituo hicho pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 132 kutoka Mkata kwenda Kilindi. mkoani Tanga

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi, amezindua pia ujenzi wa njia za kusambaza umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 45 kutoka kituo cha Mkata kwenda kijiji cha Kwamsisi.

Akizungumza na wakazi wa Mkata waliofika kushuhudia tukio hilo leo (Ijumaa, Februari 13, 2026), Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi afuatilie malipo ya hati ya madai ya zaidi ya sh. bilioni moja ya wakandarasi wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati.

 


Amesisitiza kuwa fedha ya Serikali inapotolewa inapaswa iende kufanya kazi iliyokusudiwa na akataka viongozi wasimamie matumizi ya fedha hizo. “Wakandarasi wote nchini wanapaswa kuhakikisha kuwa kiasi cha fedha kilipokelewa kiendane na kazi inayofanyika,” amesisitiza.

“Waziri wa Nishati fuatilia fedha hizo za wakandarasi ili zije haraka. Tunataka mradi wa umeme ukamilike, uende kule Kwamsisi ili viwanda vilivyopo kule vifanye kazi,” amesema.


Mapema, Waziri wa Nishati alisema ujenzi wa kituo hicho unatarajiwa kugharimu sh. bilioni 44 ambazo zitatumika kujenga kituo hicho cha kupoza umeme na kuweka tranforma mbili

Alisema Serikali imetoa sh. bilioni 73 kwa ajili ya mradi wa umeme wa REA katika vitongoji 559 kote nchini. “Hii ni awamu ya kwanza kwani tayari kuna vitongoji 4,553 nchini kote ambavyo tayari vina umeme sawa na asilimia 64 ya lengo la serikali.”

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange alimweleza Waziri mkuu kwamba ujenzi wa mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya kuimarisha gridi ya Taifa (maarufu kama Gridi Imara) ambapo serikali imetoa sh. bilioni 1.97 kugharimia miradi 27 ya aina hiyo kote nchini.

“Mradi huu ni miongoni mwa miradi ya uimarishaji wa Gridi ya Taifa wenye lengo la kuimarisha upatikanaji wa umeme katika wilaya za Handeni na Kilindi pamoja na kuimairisha hali ya upatikanaji wa umeme katika migodi ya graphite katika kijiji cha Kwamsisi,” alisema.

Akielezea faida za mradi huo, Bw. Twange alisema kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Wilaya za Handeni na Kilindi; kutawezesha upatikanaji wa umeme kwenye eneo la migodi ya graphite hivyo kuongeza uzalishaji na kuchochea uchumi na kuongeza mapato kwa shirika hilo kupitia wateja wakubwa wanaotarajiwa kupatiwa huduma hiyo.

Mradi huo unafadhiliwa na Serikali ambapo sh. bilioni 44.14 ni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme na shilingi bilioni 5.75 ni kwa ajili ya ujenzi wa njia ya kusambaza umeme.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top