Na Angela Sebastian; Bukoba
Mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali Yahya Ramadhan Kido ametaja vipaumbele vyake ambavyo ataanza navyo katika utekelezaji wa majukumu yake.
Amesema kipaumbele cha kwanza ni kuimalisha ulinzi na usalama wa mkoa huo kwa gharama yoyote na nguvu zake zote.
Kanali Kido ameeleza hayo leo katika hafla ya makabidhiano ya ofisi baina yake na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa huo Hajati Fatma Mwassa katika ukumbi wa mikutano wa mkuu huyo mjini Bukoba.
"Katika uongozi wangu nitahakikisha naendeleza ulinzi katika mkoa huu kwa sababu upo mpakani, suala hilo litakuwa kipaumbele changu namba moja katika Taifa letu nitashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuimalisha ulinzi wa mkoa wetu kama nilivyoelekezwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan wakati akituapisha Februari tisa mwaka huu kwani tupo mipakani"ameeleza Kido.
Pia ametaja kipaumbele kingine kuwa ni kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi yote inayotekekezwa katika maeneo yote ya mkoa huo na inayopangwa kutekelezwa ili thamani yake iendane na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi hiyo.
Kwa upende wa Mkuu wa mkoa mstaafu Hajat Fatma Mwassa amesem kwa kipindi cha Novemba 2024 hadi November 2025 wahamiaji haramu 17,200 waliingia Kagera kinyume cha sheria na kukamatwa kisha kurudishwa katika nchi zao.
Mwassa amesema idadi hiyo ni kubwa hivyo akamshauri kanali Kido kuangalia na kuvalia njuga suala hilo kwani mkoa wa Kagera unapakana na nchi nne.
Amesema asilimia 85 ya wahamiaji haramu hao ni kutoka katika nchi ya Burundi,asilimia tano kutoka Rwanda,asilimia tano kutoka Uganda na zilizobaki ni nchi nyingine Afrika.






