_▪️Afungua jengo la ICU Hospitali ya Handeni_
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa onyo kwa Watanzania kutoruhusu ufa wa kubaguana kutokana na majukumu waliyonayo kwa kufanya hivyo kutaharibu nchi.
“Tusiingize ufa wa kubaguana kwa kazi zetu, hiyo siyo nchi yetu tuliyoachiwa. Mkulima asimbague mfugaji wala mfugaji asimbague mkulima. Tusiruhusu ufa wa kubagua kufanya hivyo kutaharibu nchi yetu,” amesema.
Ametoa wito huo leo (Ijumaa, Februari 13, 2026) kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wakazi wa Mkata na pia wakazi wa Handeni mara baada ya kukagua na kufungua jengo la ICU katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Handeni mkoani Tanga.
Waziri Mkuu alitoa onyo hilo huku akitahadharisha kwamba idadi ya watu inaongezeka kila siku, idadi ya mifugo inaongezeka lakini ardhi haiongezeki na kwamba suala la kupanga matumizi bora ya ardhi haliepukiki.
“Wakulima ni Watanzania, wafugaji ni Watanzania. Mtu anaruhusiwa kwenda kuishi popote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili mradi havunji sheria. Tunaruhusiwa kwenda kuishi popote lakini tuepuke migogoro inayoweza kujitokeza.”
“Ili tuenzi amani ya nchi yetu, kosa la mfugaji mmoja lisiwe kosa la wafugaji wote kwa sababu tunayo jamii ya watu ambapo unakuta mtu anayelima ndiye anayefuga au anayefuga ndiye anayelima. Tusinyooshe kidole kwa mfugaji au mkulima. Ni sehemu chache sana unaweza kukuta kuna wakulima tu na wafugaji tu,” amesema.
Amesema katika miaka ya nyuma ilikuwa ikitokea bahati mbaya mfugaji ameingiza mifugo kwenye shamba la mtu, anaenda kutoa taarifa na masuala yalikuwa yakiamuliwa kidugu. “Sasa hivi imekuja hii tabia ya kiburi, ya kuingiza mifugo kwenye shamba la mtu na kumuumiza. Hatuwezi kuruhusu hili. Hatuwezi kuruhusu watu wavunje sheria halafu watumie jeuri kuwaumiza wengine.”
“Tunataka watu waishi wakiheshimu sheria, wakiitana ndugu. Tanzania ndiyo nchi tuliyoachiwa na wazee wetu, tuheshimu taratibu. Huu utaratibu wa kiburi siyo asili ya nchi yetu. Serikali haiwezi kuvumilia watu wanaoishi kwa kiburi,” amesisitiza.
Amesisitiza haja ya viongozi kuendelea kusisitiza amani na wananchi kuendelea kuitunza amani kwani mipango yote ya maendeleo inayopangwa haiwezi kutekelezwa kama hakuna amani.
Mapema, Waziri Mkuu alikagua na kufungua jengo la wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Handeni mkoani Tanga ambalo ujenzi wake umegharimu sh. milioni 426.
Waziri Mkuu alielezwa kwamba kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo kutapunguza adha kwa wakazi wa Handeni ambao ili kupata huduma, walikuwa wakilazimika kusafiri kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga iliyoko km. 160 kutoka Handeni.
Wakati huohuo, Waziri wa Kilimo, Godfrey Chongolo amesema kuwa Serikali imetoa sh. bilioni 2.5 kujenga kituo cha uchakataji mkonge kilichopo Handeni ili kukabiliana na changamoto ya uchakataji wa zao hilo.
Alisema lengo la serikali ni kuchakata tani nane za nyuzi za mkonge kwa siku pindi kituo hicho kitakapokamilika.
Naye Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema Serikali ya awamu ya sita imetoa sh. bilioni 171 kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa maji ambao kwa saa umefikia asilimia 70. “Huu ni mradi mbadala wa ule wa zamani wa HTM ambao umechakaa. Pia kuna mradi wa wa maji wa kutoka Segera hadi Kabuku ambao unajengwa kwa gharama ya sh. bilioni 25 na sasa umefikia asilimia 60.”
Waziri Mkuu kesho anaendelea na ziara yake wilayani Kilindi na Korogwe.




