Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Butiama Mhe. Jumanne Sagini amehudhuria Uzinduzi wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Butiama ambapo amemnadi na kumuombea kura za ndio Mgombea wa Urais kupitia tiketi ya CCM Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Mgombea ubunge wa Jimbo la Butiama Mhe. Dkt. Wilson Charles Mahera.
Mhe. Sagini ameeleza kuwa kuna kila sababu ya mwananchi wa Butiama kumpa kura ya ndio Mgombea wa urais, ubunge na udiwani anayetokana na Chama Cha Mapinduzi ili kutengeneza muunganiko wa mafiga matatu ambayo yatarahisha kuleta maendeleo kama yalivyopatika katika kipindi chake cha 2020-2025.
"Kipindi cha Mwaka 2020 Wilaya ya Butiama tuliongoza kutoa kura nyingi za Rais Mwaka 2025 tunaye Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Wilson Mahera pamoja na madiwani wa Kata zote 18 wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi msifanye kosa wapeni kura nyingi za ndio ili wanapoongea lugha moja maendeleo yanajaa ndani ya Butiama kwani Mhe. Rais Samia ni mtu wa huruma na nyie ni mashuhuda hatukua na Chuo Kikuu leo tunacho, mradi mkubwa wa maji mugango Kiabakari Butiama umeanza, Barabara zimefunguka umeme pia umefika maeneo mengi, shule za sekondari na msingi zimejaa Butiama," amesema Mhe. Sagini.
Mgeni Rasmi katika hafla hiyo Ndg. Joshua Mirumbe ambaye ni Katibu wa NEC, Uchumi na fedha CCM amewaomba wananchi kuendelea kuamini Chama Cha Mapinduzi kwani hakiwezi kuleta kiongozi ambaye sio sahihi hivyo ifikapo Oktoba 29 zoezi ni moja la kwenda kutiki kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ili awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Dkt. Wilson Mahera awe Mbunge wa Jimbo la Butiama pamoja na madiwani wa Kata zote 18.
Aidha Mgombea ubunge Jimbo la Butiama Mhe. Dkt. Wilson Mahera amekipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kumuamini na kuahidi kama akichaguliwa kuwa Mbunge atahakikisha anaendeleza yale yaliyofanywa na mtangulizi wake Mhe. Jumanne Abdallah Sagini na kutelekeza ilani ya chama hiko kama kinavyoelekeza.