Tukio la maafisa wa Jeshi la Polisi kuwashambulia na kuwapiga baadhi ya viongozi na makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliokuwa wamefika kwenye viunga vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Wakili Tundu Lissu leo, Jumatatu Septemba 15.2025 limeendelea kulaaniwa na wadau mbalimbali
Mwandishi wa Habari Mwandamizi na Mkurugenzi Mwenza wa Gazeti la Jamhuri Manyerere Jackton naye amelaani vikali tukio hilo, ambapo ameeleza uchungu uliopo kuona Jeshi la Polisi linageuka chombo cha mateso kwa raia wasiokuwa na hatia, tena wakifanyiwa ukatili wakiwa kwenye viunga vya Mahakama
Amesema maafisa wa Jeshi la Polisi wanapaswa kufahamu kuwa wao ni sehemu ya jamii, na kwamba haikubaliki kuona wakitumia nguvu kuwapiga ndugu na jamaa zao, kama sio Watanzania wenzao
Manyerere amesema Tanzania kama Taifa, linapaswa kufahamu kuwa kukandamizwa kwa sauti ya wananchi kwenye Taifa lolote lile kunaweza kusababisha uwepo wa mlipuko wa ghadhabu ambao hauwezi kuzimwa na risasi wala virungu
"Nepal na mataifa mengine mengi yameshuhudia maumivu ya uonevu yakibadilika kuwa mlango wa mapinduzi ya wananchi, je sisi hatujifunzi?, nani katuroga?, Polisi sio maadui zetu, wao ni walinzi tuliowakabidhi dhamana ya maisha yetu, lakini wanapogeuka na kuwa silaha za kupiga, kujeruhi na hata kuua tunabaki kujiuliza, Tanzania inaelekea wapi?, Taifa letu halihitaji risasi wala mabavu kulinda heshima yake, bali haki, heshima ya utu na huruma" -Manyerere
Aidha, Manyerere ametoa wito kwa wadau wote nchini kusimama kidete na kusema sasa hatutaki tena kuumizana, kwani haki si zawadi, bali haki ni ya kila mmoja hivyo maafisa wa Jeshi la Polisi waache kutumia nguvu kuumiza raia wasiokuwa na hatia
Sambamba na hilo, ametoa wito kwa serikali kuwawajibisha wahusika, huku wananchi wakiendelea kusimama kidete kudai amani yenye usawa na haki, na si amani ya hofu kwakuwa mwisho wa yote Tanzania ni ya kila mmoja, na kwamba hata siku moja hatuwezi kuijenga kwa maumivu ya miongoni mwetu, kwakuwa nayo yana mwisho.