Hekaheka za mchujo CCM:
Sababu ya wabunge nguli kufyekwa na wajumbe hizi hapa
*Yadaiwa walikuwa bize na wananchi wakasahau 'kuwaona' wajumbe wa kamati za siasa
*Wajumbe wengine walia kupunjwa mgao
BAADHI ya kamati za siasa za chama cha mapinduzi CCM za wilaya nchini zinadaiwa kukiuka taratibu za chama hicho za kuwapata viongozi wa dola kwa madai ya kupokea rushwa jambo ambalo liliwafanya kuendesha vikao vyao kwa upendeleo mkubwa,chuki na fitna.
Uchunguzi ambao umefanywa katika baadhi ya mikoa nchini umebaini kuwa baadhi ya viongozi wa kamati hizo hasa wenyeviti na makatibu walinunuliwa kabla ya kuanza kwa vikao hivyo vya mapendekezo kwa wagombea ubunge na udiwani.
Imeelezwa kuwa chanzo cha viongozi hao kununuliwa na baadhi ya wana ccm waliokuwa tayari wamejipanga kuchukua fomu ni kutokana na baadhi ya wabunge kushindwa kuwajali binafsi badala yake walitumia muda mwingi kwa shughuli za maendeleo pamoja kuwalinda wajumbe katika maeneo hayo.
Imeelezwa kuwa kutokana na wabunge kushindwa kuwapa maelezi iliwalazimu kuingia mikataba na baadhi ya wana ccm walionesha nia ya kugombea ubunge katika maeneo yao hivyo kuwasaliti wabunge walikuwepo madarakani hatua ambayo ilizua migogoro mingi kati ya wabunge na viongozi hao.
"Kaka si ni binadam,tulienda mkutano mkuu Dodoma wilaya yetu inajimbo zaidi ya moja,lakini tumekaa siku zote hatukuona mbunge hata mmoja kutukaribisha chakula na wao walikuwa hapo hapo Dodoma,tulifadhiliwa sana na baadhi ya makada ambao leo wamechukua fomu za ubunge hivyo unatarajia sisi tumpendekeze kwenye kikao chetu?yeye alidhani sisi tunakula madarasa au zahanati zake?tumewafyeka ngoja waponee huko sio kwetu"alisema mmoja ya kiongozi katika moja ya wilaya mkoani Mara.
Aliongeza kuwa"Huwezi kumpendekeza mtu eti kwa vile wananchi wanamhitaji, je sisi tufe njaa? Tumesema tupo tayari kwa lolote lakini hatuwezi kuwapendekeza kwenye kikao chetu.
Mjumbe huyo alisema wanafahamu fika kwamba huenda uamuzi wao ukawasababishia machungu katika uchaguzi ujao wa viongozi wa Chama mwaka 2027.
"Tutunajua 2027 ni vita lakini tumesema potelea mbali, tunataka kuonesha mfano"aliongeza.
Hata hivyo katika sakata hilo imebainika kuwa baadhi ya wajumbe wa kamati hizo za siasa ngazi ya wilaya kupunjwa mgao wa fedha zilizotolewa na watia nia.
Wamesema pamoja kuwa wameshiriki katika mchezo huo lakini wamejutia kuingizwa katika vita ambayo hawakuitegemea kwa sasa.
"Kweli mimi ni mjumbe tulipewa maelekezo na mkubwa wetu kuwa kuna fedha tutapata mimi nimeambulia milioni mbili huku viongozi wetu wakigawana milioni 20 kila mmoja, najuta kwa nini nimeshiriki katika kitendo hiki"alisema mjumbe huyo wa kamati ya siasa katika moja ya wilaya mkoa wa Mara.
Kauli za baadhi ya viongozi na wajumbe hao zimeonekana kufanana kwa baadhi ya maeneo nchini, jambo ambalo ni hatari na linaweza kusababisha madhara makubwa kwa chama hicho kinachotawala
Mzee Juma Remagwe wa wilaya ya Tarime alisema kuwa vitendo hivyo vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi na watendaji wa CCM kwa maslahi binafsi vinaweza kusababisha chuki kwa wananchi kwa kuchaguliwa viongozi wao na kikundi cha watu wachache. Alisema hatua hiyo inaweza kuleta madhara makubwa kwa chama siku za usoni.
"Ndugu Mwandishi CCM hii sio ile ya Nyerere kuna viongozi wamepewa nafasi kumbe ni majizi kabisa, unawezaje kuharibu sifa za chama kwa maslahi yako binafsi,hivi kama kingekuwa ndio kikao cha mwisho tungetarajia nini? Nadhani ufike wakati Mwenyekiti wa chama awe mkali kwa wahuni kama hawa wanaotumia kofia ya chama kufanya vitendo vichafu kiasi hiki. Mwenyekiti mzima unatembea na mtia nia mwaka mzima,unagawa rushwa za mtia nia huku mbunge yupo madarakani, lakini hatukuona hatua zimechukuliwa, sijui vyombo vyetu vya usalama havioni? Hii ni hatari kwa maisha ya chama."'alisema.
Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinadai kuwa baadhi ya wabunge wengi wanaomaliza muda wao wameshindwa kupendekezwa na vikao vya kamati za siasa za wilaya na zile za mkoa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo hizo za rushwa.
Katibu wa halmashauri Kuu ya CCM siasa, Uenezi na Mafunzo Amos Makala alipotafutwa na Mwandishi wa habari hii ili aweze kuzunguzia tuhuma hizi na hatua zinazoweza kuchukuliwa endapo ikithibitika viongozi hao kukiuka taratibu na miongozo ya chama, hakuweza kupatikana baada ya simu yake kuita bila majibu. Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi haukuweza kujibiwa. Juhudi za kumtafuta bado zinaendelea.
Tayari CCM kupitia kwa viongozi wake wakuu, wamesikika mara kadhaa wakionya vikao vya maamuzi kutenda haki na wajumbe wake kujiepusha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili, upendeleo na rushwa wakati wote wa kujadili wana CCM waliotia nia kugombea nafasi mbalimbali za dola.