MSD yawadai Bil. 6.2 watoa huduma za afya

GEORGE MARATO TV
0


Na MASHAKA MHANDO, Korogwe

BOHARI ya dawa nchini (MSD) Kanda ya Tanga, imesema inakabiliwa na changamoto ya ufanisi wa kazi kutokana na madeni inayowadai vituo vya kutoa huduma ya afya ya zaidi ya Sh. 6,242,077,935.35 katika kanda hiyo.

Akitoa  salamu kwenye kikao baina ya MSD na wadau wake, Kaimu Meneja wa bohari hiyo Kanda ya Tanga, Granty Mwapwele alisema fedha hizo zinatokana na kusambaza bidhaa za afya kwenye vituo vyote 568 vinavyohudumiwa na MSD Kanda ya Tanga katika mwaka wa fedha wa 2024-2025.

"Bohari ya dawa Kanda ya Tanga imekumbwa na changamoto ya kwa baadhi ya vituo vyote vya kutolea huduma kuwa na madeni makubwa hali hii inaathiri kiasi kikubwa huduma zetu," alisema.

Alisema MSD Kanda ya Tanga inahudumia jumla ya Halmashauri 12 zenye jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 568 kwa kusambaza bidhaa za afya mara sita kwa mwaka pale wanapohitaji.

Alitaja vituo wanavyovihudumia kuwa ni pamoja na hospitali ya rufaa Bombo, hospital ya magonjwa maalum, hospitali za wilaya, hospitali za mashirika ya dini, hospitali za majeshi, vituo vya afya na zahanati za mkoa wa Tanga na halmashauri ya wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Alisema MSD kwa mwaka wa fedha wa 2024-2025 pamoja na changamoto hiyo wamefanikiwa kusambaza bidhaa za afya zenye thamani ya sh. 22,546,511,002.97 katika vituo hivyo.

Aidha Kaimu Meneja huyo alisema kuwa MSD pia wanahusika na usambaji wa vifaa mbalimbali vya miradi ya serikali katika vituo vya kutolea huduma za afya vya mradi wa Cemon unaosimamiwa na TAMISEMI, mradi wa vyandarua na mradi wa hospitali za jeshi.

Alisema usambazaji huo wa vifaa tiba kwa fedha za ruzuku kutoka TAMISEMI ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2024-2025 wamefanikiwa kusambaza vifaa vyenye thamani ya sh. 2,855,028,969.66.

"MSD inafanyakazi pamoja na Wizara kuhakikisha bidhaa za afya na vifaa tiba vinavyohitajika vinapatikana na kufikishwa kwa haraka pale vinavyohitajika," alisema na kuongeza MSD inatarajia kuboresha mnyonyoro wa ugavi kwa faida ya Watanzania wote.

Aliwaeleza wajumbe pamoja na mgeni rasmi umuhimu wa kukukata katika kikao hicho kujadili changamoto wanazokabiliana nazo katika utendaji wa Kila siku ili waweze kuboresha huduma za afya kwa faida ya wananchi.

Awali akifungua kikao hicho, kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batlida Burian, Mkuu wa wilaya ya Korogwe William Mwakilema alimuagiza mganga Mkuu wa mkoa wa Tanga (RMO) kusimamia ukusanyaji wa mapato katika vituo vya kutolea huduma  ili fedha zinazopatikana katika uchangiani ziweze kulipa madeni ya MSD kwa wakati.

"RMO simamia ukusanyaji wa mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya ili vituo viweze kulipa madeni ya MSD kwa wakati mara baada ya kupokea shehena ya bidhaa kuepuka madeni yasiyokuwa na lazima,"alisema.

Mkuu wa mkoa alimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha katika sekta ya afya ili kuboresha huduma za afya nchini.

Pia amewakumbusha wadau wa mkutano huo kuhakikisha wanafanyia kazi kwa usahihi matokeo ya bidhaa za afya ili MSD waweze kuwa na takwimu sahihi zitakazowasaidia kuagiza bidhaa hizo na kuzisambaza kwa haraka.

Mkuu wa mkoa aliwaagiza kuhakikisha jukumu waliokuwa nalo la kusimamia vituo vya afya katika maeneo yao wanasimama mapato yanayopayikana katika uchangiaji huduma ili waweze kununua bidhaa afya pamoja na kusimamia mnyororo wa ugavi wa bidhaa hizo.

Mkutano huo umewakutanisha waganga wakuu wa hospitali za wilaya, wafamasia, fundi sanifu vifaa tiba, wataalamu wa maabara na watumishi wa MSD.











Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top